sedoyeka
Mume na mke wakulima na wakazi wa kijiji cha Tambukareli, Tarafa ya Itigi, wilaya ya Manyoni mkoani Singida, wameuawa kikatili kwa kukatwa katwa kwa mapanga sehemu mbali mbali za miili yao na watu wasiofahamika.

Wanandoa hao ni Mbulalina Shomi (80) na mke wake Joyce Mathayo (70), ambapo inadaiwa kuwa wameuawa na mtoto wa kambo Henry Yoweli Malugu (55) ambaye ni mtoto wa marehemu Joyce Mathayo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo la kusikitisha, limetokea Aprili, 10 mwaka huu saa sita za usiku huko katika kijiji cha Tambukareli.

Alisema siku ya tukio wakati wanandoa hao wamelala, walivamiwa na watu wasiofahamika baada ya kuvunja mlango wa mbele wa nyumba yao na kuingia ndani na kutekeleza azma yao.

Sedoyeka alisema uchuguzi wa awali umebaini kuwa muuaji huyo  wanawania mifugo mingi ambayo idadi yake haijafahamika,iliyokuwa inamilikiwa na marehemu Mbulalina.

Alisema wanamshikilia Henry na baada ya kumaliza upelelezi, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

Katika tukio la pili,Kamanda huyo alisema wanawashikilia Wende Makoye (28) na Gidangida Ganagu (30) wakazi wa kitongoji cha Midimbwi kijiji cha Munguli, Tarafa ya Kirumi, Wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida,kwa tuhuma ya kumiliki lita 20 za pombe haramu ya Moshi/Gongo.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakati wa msako wa kukamata watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Wakati huo huo, Sedoyeka alisema kuwa jumla ya bunduki aina ya Rifle 30, Bastola 35 na shotgun,zimeisha hakikiwa kati ya aprili mosi na sasa.

“Changamoto inayoendelea kujitokeza katika zoezi hili la kuhakiki silaha,ni muitikio mdogo wa wananchi kutokana na upatikanaji wa taarifa inayosababishwa na hali ya kijiografia ya mkoa wetu,” alisema.