Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Waziri wake, Mhe. Ummy Mwalimu imeeleza kuwa inajipanga kufanya utafiti ili kuona ni jinsi gani wataweza kumaliza ugonjwa wa Kipindupindu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Ummy Mwalimu amesema haikuwahi kutokea awali kwa Kipindupindu kuwepo nchini kwa kipindi kirefu kama ilivyo sasa na hivyo wameona ni vyema kufanya utafiti kuona kwanini ugonjwa huo bado unaendelea kuwepo nchini.

Amesema utafiti huo utafanyika kwa kipindi cha wiki sita na baada ya hapo watazishirikisha ofisi zilizo juu ya wizara hiyo ili kuona ni jinsi gani wataweza kusaidiana kumaliza Kipindupindu.
Ummy Mwalimu
Waziri Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu.

“Haikuwahi kutokea kipindupindu kuwepo nchini kama ilivyo sasa kilikuwa kikikaa sana nchini ni miezi miezi miwili au mitatu lakini hiki cha sasa hivi kinakaribisa miezi saba sasa kwahiyo tumeona kwanza tufanye utafiti,

“Baada ya utafiti tutashirikisha ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya rais na hapo tutaona ni hatua gani itachukuliwa kwa pamoja tukishirikiana,” amesema Mhe. Mwalimu katika mkutano huo.

Aidha ameeleza kuwa wagonjwa wapya wa Kipindupindu kwa kuanzia Aprili, 4 hadi 10 wamepungua kutoka 531 kwa wili iliyotangulia hadi kufikia 368, na mkoa wa Mara ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa 128 na kifo kimoja huku mikoa ya Njombe na Ruvuma ikiendelea kuwa salama kwa kutokuripoti mgonjwa yoyote.
Watumishi Wizara ya Afya
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto waliohudhuria mkutano wa Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu na waandishi wa habari.
DSC_0054
Waziri Ummy akizungumza na waandishi wa habari.