MBUNGE
wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ushauri ya masuala ya Ukimwi, Afya ya Mama na Watoto ya
Taasisi ya Mabunge Duniani (IPU). Dk Ndugulile amechaguliwa katika
mkutano wa 134 wa Mabunge duniani unaoendelea mjini Lusaka, Zambia.
Mkutano
huo ulioanza Machi 17, mwaka huu unatarajia kuisha keshokutwa. Kabla ya
kuchaguliwa kwake, Dk Ndugulile alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa kamati
hiyo.
Kamati
hiyo inajumuisha wabunge wasiozidi 12 ambao huteuliwa na Rais wa IPU
kutokana na umahiri na mchango wao katika masuala ya Ukimwi na masuala
ya afya ya mama na watoto.
Wajumbe
wengine wa kamati hiyo wanatoka nchi za Armenia, India, Bangladesh,
Afrika Kusini, Rwanda, Italia, Ubelgiji, Austria, Sweden, Dominica na
Marekani.
Majukumu
ya Kamati hiyo ni kushauri, kujengea uwezo na kuhamasisha mabunge
duniani kuhusiana na njia bora za kuboresha huduma za Ukimwi pamoja na
afya za akinamama na watoto.
Dk
Ndugulile ni daktari bingwa katika magonjwa ya maambukizi na pia kwenye
afya ya jamii. Pamoja na majukumu hayo mapya, pia mbunge huyo ni
Mwakilishi wa bara la Afrika katika Taasisi ya Kimataifa ya Ukimwi,
Mjumbe wa Kamati ya Wabunge Duniani kuhusu masuala ya Kifua Kikuu (TB)
na Mwakilishi wa Bunge la Tanzania kwenye Bunge la Afrika.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment