NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

ICELAND IWE FUNDISHO KWA TANZANIA


Iceland 2
Kwenye dunia ya michezo, miaka ya nyuma ilikuwa ni story kubwa sana kushuhudia mataifa ambayo hayakupewa nafasi au hayakuwa namajina makubwa kwenye tasnia ya soka kupata matokeo dhidi ya timu vigogo au zenye majina makubwa na kusheheni wachezaji maarufu kwenye soka la ulimwengu huu.

Timu ya taifa ya Cameroon iliwahi kufanya maajabu na kuushangaza ulimwengu kwenye michuanoano ya kombe la dunia zilizofanyika Italy, wawakilishi hao wa Afrika walimchapa bingwa mtetezi (wakati huo) Argentina kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa ufunguzi na hawakuishia hapo, jamaa hawa walitinga hadi hatua ya robo fainali.

Jambo hili liliutikisa ulimwengu na Cameroon ikaingia kwenye historia mpya kwenye vitabu na kumbukumbu za soka.

Mwaka 2002, Senegal wakarudia kile ambacho kilifanywa na Cameroon. Walianza kwa kumfunga aliyekuwa bingwa mtetezi Ufaransa kwa goli 1-0 nao wakafika hadi hatua ya robo fainali.

Bulgaria walifika nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia, hii ilikuwa ni mwaka 1994.

Kwenye historia ya fainali za Euro, mwaka 2004 Ugiriki nao waliishangaza dunia licha ya kuwa timu iliyopewa nafasi ya mwisho kati ya timu zote ambazo zilikuwa zikishiriki michuano ya mwaka huo.

Ugiriki ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa Euro mwaka 2004 kwa kuifunga mara mbili timu ya taifa ya Ureno iliyokuwa imesheheni nyota kibao waliopewa jina la kizazi cha dhahabu kutokana na kuundwa na nyota waliotamba barani Ulaya kama vile Costa, nahodha Luis Figo, Pauleta, Deco, Cristiano Ronaldo ndiyo alikuwa ikiibuka enzi hizo.

Mwaka 1992 Denmark ilishiriki fainali za Euro ikienda kuchukua nafasi ya Yugoslavia ambayo ilikuwa imeondoshwa mashindanoni kwasababu wakati huo wao walikuwa wakipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ikumbukwe kwamba, Denmark walipewa taarifa siku 10 kabla ya michuano hiyo kuanza.

Wakaenda Sweden kushiriki fainali hizo na kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa kuifunga Ujerumani bao 2-0 katika mchezo wa fainali.

Hizi ni story kubwa ambazo zilitikisa ulimwengu kwa timu ambazo hazikupewa nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano husika kutokana na udogo au uwekezaji uliofanywa na mataifa husika kwenye mchezo wa soka.

Turudi kwenye pointi yangu ya msingi ambayo leo nataka nikumegee, sikuhizi mambo yamekuwa tofauti kidogo, wakati ule mataifa yaliyokuwa hayajaendelea kwenye mchezo wa soka yalipofanya vizuri ilikuwa ni jambo la kushangaza kwasababu ya aina ya uwekezaji uliokuwa unafanyika.

Mataifa mengi yalikuwa hayajaendelea kwenye mchezo wa soka kwahiyo ilikuwa ni kitu cha kustaajabisha kwa taifa ambalo halikuwa na miundo mbinu bora, hakuna makocha wazuri, wala hakuna ligi bora. Watu walikuwa wanajiuliza swali moja kubwa, haya mataifa yanapata wapi jeuri ya kushindana na kupambana na mataifa ambayo yalishapiga hatua tangu zamani?

Siku hizi mambo ni tofauti kabisa hususan baada ya utawala wa Sepp Blatter na hapa ndipo rais huyu wa FIFA alipoacha alama kwenye uongozi wake. Ukiachana na mabaya yake, Blatter alijitahidi kupunguza gap kati ya anayejua na asiyejua, na matokeo yake tumeanza kuyaona sasahivi kwa mataifa madogo kama Albania, Iceland na mengine kupata matokeo na kusumbua mataifa makubwa ambayo yalikuwa yanahistoria kubwa katika mchezo wa soka.

Sasahivi underdogs imebaki Tanzania pekeyake, kwasababu hadi Afrika kunamatokeo ya kushangaza kwenye ulimwengu wa soka. Hivi karibuni, visiwa vya Comoro viliilazimisha Ghana sare ya bila kufungana lakini kwa upande wetu sisi Tanzania tumebaki kuwa underdogs kwa kushindwa kupata matokeo kwasababu ya kushindwa kujifunza kutoka kwa wenzetu nini wanafanya.

Sikuhizi watu wanafanya uwekezaji sahihi kwenye mchezo wa soka, wanawekeza kweli kwenye soka la vijana kwa kutengeneza miundombinu ya kutafuta ijana wenye vipaji vya kweli, kuviendeleza na kuvipa-exposure ili viweze kwenda mbele kama vile Iceland walivyoweza kufanya kwa nyota wao Gylfi Sigurdsson mchezaji ambaye ndiye nyota wa timu yao.

Baada ya kugundua kipaji chake, wakampeleka England kwenye academy ya Reading akiwa bado bwana mdogo ili apate kuonekana na kushindana na vijana wenye vipaji vinavyolingana na chake, leo hii anacheza ligi ya England na ndiyo anaisaidia timu yake ya taifa.

Lakini hapa nyumbani tayari mashindano kwa shule za msingi na sekondari (UMITASHUMTA na UMISETA) tayari yamepigwa pini, sitaki kulijadili sana hilo maana tatizo letu watanzania hatupendi kuambiwa ukweli na mtu hugeuka adui mara tu anapozungumza ukweli. Lakini nakumbuka waswahili wanamsemo wao unasema, ‘dawa ya homa kali ni sindano japo inauma’.

Kwakifupi kama tunataka kufanikiwa katika michezo, hakuna uchawi, mazingaombwe wala miujiza, ni kutafuta namna nzuri ya kuwekeza na hiyo ndiyo italeta matokeo chanya kama mataifa mengine madogo ambayo tunayaona yakifanya vizuri hii ni kutokana na uwekezaji ambao waliufanya.

Tukiwa na viongozi thabiti wenye nia ya dhati kuendeleza michezo yetu na sio wale wajanja-wajanja na wahuni hakuna haja ya kueleza mengi katika hili kwasababu kilakitu kipo wazi.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment