Mahakama
Kuu Kanda ya Moshi, imemfunga jela maisha mfanyabiashara, Silay Maulid
Jumanne (35) baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 21 za
majani ya mirungi.
Hukumu hiyo iliyotolewa jana na Jaji Mfawidhi
wa mahakama hiyo, Aishiel Sumari, ni ya kihistoria katika vita dhidi ya
dawa za kulevya nchini kwani haijawahi kutolewa tangu Tanzania ipate
Uhuru.
Wengi wa wanaokamatwa na mirungi, hushtakiwa kwa kupatikana na
mirungi, shtaka ambalo husikilizwa na mahakama za chini tofauti na
kusafirisha ambalo husikilizwa na Mahakama Kuu.
Kutokana na
mazoea hayo, washtakiwa wengi wanaopatikana na hatia kwa kosa la
kupatikana na mirungi, huishia kupigwa faini hatua inayoelezwa kuchangia
kushamiri kwa matumizi ya mirungi.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo
jana hakuamini masikio yake pale Jaji Sumari alipomweleza kuwa adhabu ya
kusafirisha mirungi kama ilivyo dawa nyingine za kulevya ni kifungo cha
maisha jela.
Akitoa adhabu hiyo, Jaji Sumari alisema upande wa
mashtaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme
umejenga kesi hiyo na kuishawishi Mahakama pasi na kuacha shaka.
Upande
wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mndeme akisaidiwa na mwenzake Kassim
Nassir, ulidai kuwa Septemba 7, 2013, mshtakiwa alikamatwa na vifurushi
21 vya Mirungi.
Kwa mujibu wa mashtaka hayo, mshtakiwa
alikamatwa kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi, akiwa kwenye harakati za
kusafirisha mirungi hiyo kwenda kuiuza jijini Arusha.
Jaji
Sumari alisema ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashitaka,
umethibitisha kuwa mshtakiwa alikamatwa na begi la rangi ya kijani
likiwa na mirungi hiyo.
Alisema licha ya mshtakiwa aliyekuwa
akitetewa na Wakili Martin Kilasara, kujitetea kuwa hakukamatwa stendi
kuu bali eneo la Majengo mjini Moshi, ushahidi umethibitisha alikamatwa
stendi kuu.
“Baada ya kusikiliza ushahidi, mashahidi
wamethibitisha ulikamatwa Stendi Kuu Moshi, ushahidi huo uliungwa mkono
na kondakta wa basi na dereva teksi aliyekuchukua,” alisema.
Jaji
Sumari alisema polisi hawakuwa na sababu yoyote ya msingi ya
kumbambikia shtaka mshtakiwa huyo, kama alivyojaribu kujitetea na
kusisitiza kuwa ushahidi ulikuwa madhubuti dhidi yake.
“Kulikuwa
na tofauti ndogondogo kama begi lilibebwa na nani kutoka stendi, au
kutoka kwenye basi kwenda kwenye teksi lakini zilikuwa ni tofauti ndogo
hazikuharibu mizizi mikuu ya ushahidi,” alisema.
Kwa mujibu wa
Jaji Sumari, ukiacha ushahidi huo, ungamo la mshtakiwa linaongeza nguvu
na kushabihiana na ushahidi uliotolewa na mashahidi.
Jaji Sumari
alisema mirungi ni dawa za kulevya zenye madhara, ushahidi wa Mkemia
Mkuu wa Serikali, ulibainisha matumizi yake humfanya mtumiaji kuwa
mtegemezi wa dawa hizo.
“Matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri
jamii ulim wengu mzima hasa vijana, hivyo sheria hii ilitungwa
ikizingatia uhai wa binadamu ndiyo maana imeweka adhabu kali,” alisema.
Jaji
Sumari alimweleza mshtakiwa huyo ambaye muda wote alikuwa akijifuta
jasho na kunywa maji, kuwa mtu yeyote anayepatikana akisafirisha mirungi
na dawa nyingine ni kufungwa jela maisha.
Hukumu hiyo
ilionekana kuwa gumzo katika viunga vya mahakama hiyo jana, huku
wanasheria wakisema inapeleka ujumbe kwa jamii kutodharau kosa
linalohusiana na mirungi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS) Tawi la Moshi, David Shilatu alisema hukumu hiyo ni ya
kwanza kutolewa na ya aina yake Tanzania.
“Kwa sheria zetu hizi
na marekebisho yake, mirungi nayo inaangukia daraja la dawa za kulevya,
kwa hiyo upande wa mashtaka ukithibitisha ulikuwa unasafirisha adhabu ni
kubwa,” alisema Wakili Shilatu.
Shilatu alisema ingawa
mshtakiwa anayo haki ya kukata rufaa, lakini hukumu hiyo itoshe kupeleka
ujumbe kwa jamii kwamba matumizi ya mirungi na usafirishaji wake ni
kosa la jinai nchini.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment