Baada ya Arsenal kuvurunda huenda Leceister City akawa bingwa EPL
Baada ya mechi za jana usiku za ligi kuu ya England, hatimaye zimebaki takribani mechi 10 kabla ligi hiyo kumalizika, na hali inaonyesha inazidi kuwa mbaya kwa vigogo wa ligi.
Hii imekuja baada ya klabu ya Arsenal na wapinzani wao wa London ya kaskazini Tottenham Hotspur wote kupigwa katika mechi za usiku wa kuamkia leo huko England.
Arsenal baada ya kunyooshwa na Manchester United wikiendi iliyopita leo waliwakaribisha Swansea ambao nao wamekuwa na mfululizo wa matokeo mabovu.
Joel Campbell alianza kuifungia Gunners goli la mapema dakika ya 15 ya kipindi cha kwanza, lakini goli hilo likadumu kwa dakika 17 na Routledge akaisawazishia Swansea na timu zikaenda mapumziko 1-1.
Kipindi cha pili Arsenal wakaendelea kupelekeshwa na Swansea na dakika ya 74, nahodha wa Swansea Ashley Williams akaifungia timu yake goli la ushindi katika dimba la Emirates.
Umbali kidogo kutoka kwenye uwanja wa Emirates, pale Upton Park, West Ham ambao nao wanaisaka nafasi ya 4 wakiwa nyuma na Man United, walifanikiwa kuisimamisha Tottenham wanaoshika nafasi ya pili kwenye ligi.
Goli pekee la Antonio dakika ya 7 ya mchezo lilitosha kuwapa ushindi muhimu vijana wa Slaven Bilic mbele ya kikosi cha Pochettino.
Kwa matokeo hayo ya vigogo vya London, Spurs na Arsenal wamepoteza nafasi ya kuisogelea Leceister City kileleni baada ya jana ‘Mbwa Mwitu’ kutoka sare ya 2-2 na West Brom.
Leceister anaendelea kuongoza ligi hiyo akiwa na pointi 57, Spurs anamfuatia akiwa na pointi 54, Gunners wanashika nafasi ya 3 wakiwa na pointi 51.
0 comments:
Post a Comment