NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

BODI YA MIKOPO YATOA SIKU 60 KULIPWA MADENI YAO

 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa siku 60 kuanzia tarehe 14 Machi, 2016 kwa wanufaika wote wa mikopo wanaodaiwa na HESLB kujitokeza na kuanza kulipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Bw. Jerry Sabi imesema kuwa katika muda huu wa siku 60 waajiri pia wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao waliohitimu katika vyuo vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi.

Taarifa imesema kuwa inalenga kuwakumbusha waajiri ambao bado hawatimizi wajibu wao kisheria (kifungu cha 20) wa kuwasilisha majina ya waajiriwa wao wote ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu kwa HESLB ndani ya siku 28 tangu waajiriwe.

Adhabu ya kutotekeleza wajibu huu kwa mwajiri ni faini ya shilingi milioni saba (Tshs milioni 7) au kifungo au vyote kwa pamoja na kwa mnufaika wa mkopo atashindwa kutoa taarifa hizo, adhabu yake ni kushitakiwa mahakamani.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, baada ya HESLB kupokea orodha kutoka kwa mwajiri, itafanya uchambuzi ili kubaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu na kumwelekeza mwajiri kuingiza makato ya marejesho kwenye mshahara wa mnufaika na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB.

Adhabu ya kutowasilisha makato kwa HESLB ni faini ya asilimia 10 ya makato yote ambayo hayajawasilishwa na faini hiyo inapaswa kulipwa na mwajiri.

Wajibu wa mnufaika wa mkopo na wazazi, walezi, wadhamini

Aidha, pamoja na wajibu wa mwajiri kama ulivyofafanuliwa hapo juu, wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu tangu mwaka 1994, wana wajibu wa kisheria (Kifungu cha 19 cha sheria ya HESLB), pamoja na mambo mengine, kuitaarifu HESLB kwa maandishi mahali alipo na kuandaa utaratibu wa kulipa deni lake la mkopo wa elimu ya juu.

Aidha, HESLB inapenda kuwakumbusha wazazi, walezi na wadhamini wa wanafunzi walionufaika na mikopo kuwa wana wajibu wa kisheria (chini ya kifungu cha 22 cha sheria ya HESLB) wa kuhakikisha kuwa taarifa muhimu za mnufaika waliyemdhamini zinaifikia HESLB.

 

chanzo>mpekuzi 

 

Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment