NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Kamati ya Bunge Yamchokonoa Rais Magufuli Vibali vya Sukari



KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imemwomba Rais John Magufuli kuangalia tatizo la uhaba wa sukari nchini na kuona jinsi ya kufanya kuruhusu kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuagiza sukari nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Mary Nagu alisema uhaba wa sukari nchini kwa sasa ni kati ya tani 80,000 hadi 100,000 na kwamba kama hatua za haraka hazitachukuliwa, bidhaa hiyo itahadimika na wananchi watalanguliwa.

“Tumekutana na Bodi ya Sukari, na tumezungumza nao, wametuambia kuna upungufu wa sukari ya matumizi ya nyumbani kati ya tani 80,000 hadi 100,000, tunamuomba Rais na serikali yake kuangalia jambo hili na kuona umuhimu ya kuruhusu kiasi hicho cha sukari kiingizwe,” alisema Dk Nagu.

Alisema kabla ya nchi kubinafsisha viwanda vya sukari ilikuwa inazalishwa kwa mwaka tani 100,000 na baada ya kubinafsishwa viwanda vya ndani vinazalisha tani 320,000 ilhali mahitaji ni tani 420,000.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka mataifa ya kigeni ili kuvilinda viwanda vya sukari nchini humo ambavyo vimeathiriwa na uingizaji wa sukari ya bei rahisi kutoka nje.

‘’Tuna viwanda nchini ambavyo hununua miwa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo. Viwanda hivi huzalisha sukari, ajira na ni chanzo cha mapato ya serikali. Ijapokuwa tuna hifadhi ya kutosha ya sukari kuna watu serikalini wanaotoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje,” alisema Dk Magufuli.

Aidha, Bodi ya Sukari Tanzania ilitangaza kushusha bei ya sukari kwa kutangaza bei elekezi inayoonesha bidhaa hiyo kuanzia sasa inauzwa Sh 1,800 kwa kilo nchini kote, huku ikisema haitasita kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wale watakaobainika kupandisha bei au kuhodhi bidhaa hiyo.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezekezaji, Charles Mwijage alisisitiza kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini na kuwataka wafanyabiashara walio na leseni za kuingiza na kuuza bidhaa hiyo, kutoificha.

Hata hivyo, Dk Nagu jana alidai upungufu wa sukari nchini upo na kwamba wapo wafanyabiashara wanaotumia mwanya huo vibaya kwa kuagiza sukari nyingi kuliko ile iliyokubaliwa kwa lengo la wao kunufaika, na kuiomba serikali kuongeza juhudi za kuziba mianya ya uingizaji wa sukari bila vibali.

Alisema ni vyema serikali ikaona haja ya kuondoa tatizo la uhaba wa sukari hivi sasa kwa sababu kama uhaba huo utaendelea, wananchi ndio wataathirika zaidi huku wafanyabiashara akitumia mwanya huo kuongeza bei ya bidhaa hiyo ila iwapo itaagizwa kwa wakati, si rahisi kwa wafanyabiashara hao kupandisha bei.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa cha mkoani Morogoro, Hamad Yahaya anawasihi wafanyabiashara wasio waaminifu, kuacha kutoa taarifa za uongo kuhusu kiasi cha sukari waliyonayo ili ionekane kuna upungufu na wao wapandishe bei.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment