Kasi ya kutumbua majipu imeonekana kuwatia kiwewe wakuu wa Wilaya za
Mkoa wa Kagera kwa kufanya kazi na mikutano ili kuhakikisha hakuna
makosa yatakayoonekana wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa
ya kukagua miradi ya maendeleo inayoanza kesho kutwa.
Kwa wiki
moja sasa, wakuu hao wanafanya mikutano ya kila siku na kukagua miradi
hiyo ili kuhakikisha hakuna makosa yanayoweza kusababisha kutumbuliwa
majipu.
Mkuu wa Wilaya ya Missenye, Festo Kiswaga alisema
mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa wamechukua tahadhari kwa kuhakikisha
kila eneo liko salama.
“Tunafanya maandalizi kila sehemu na idara maana ni vigumu kutabiri Waziri Mkuu atatembelea wapi,” alisema Kiswaga.
Alisema ratiba ya maeneo atakayotembelea Waziri Mkuu imebadilika mara tatu tangu walipotaarifiwa.
Mkuu
wa Wilaya ya Bukoba, Jackson Msome alisema wanalazimika kuzingatia
kanuni ya mchezo wa soka kwa kuelekeza maandalizi kila idara kuanzia
sehemu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji.
“Ni lazima kujiandaa
kila idara kufanikisha ziara ya Waziri Mkuu kwa sababu hatuwezi
kujiamini na ratiba bila kuchukua tahadhari ya ziara za kushtukiza eneo
lolote,” alisema Msome.
Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Darry
Rwegasira alisema licha ya ratiba kuonyesha kuwa Waziri Mkuu atatembelea
na kuzindua jengo la upasuaji katika kituo cha Afya cha Nyakanazi,
wamefanya maandalizi katika eneo lote ili kuepuka kushtukizwa iwapo
ratiba itabadilika ghafla.
Mfanyabiashara mjini Bukoba, Dennis
Gregory alisema wanakusudia kuwasilisha kwa Waziri Mkuu changamoto ya
bei ndogo ya kahawa inayouzwa nchini ikilinganishwa na Uganda.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment