WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa(Pichani) amesema watumishi wa umma wako huru
kuhamia kokote wapendako lakini wahakikishe wanaenda huko wakiwa safi na
kamwe mtu asiharibu kazi kazi akitarajia kuwa atahamishiwa sehemu
nyingine.
"Serikali
hii haina utumishi kwa mtu aliyeharibu kazi,usije ukaharibu hapa
Itilima ukadhani utaenda Bunda kuendelea na kazi. Serikali ya awamu hii
haina nafasi na watumishi wa aina hiyo," amesema.
Waziri
Mkuu ametoa onyo hilo leo (Ijumaa, Machi 4, 2016) wakati akizungumza na
watumishi wa wilaya ya Itilima kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya
hiyo ambao ameuzindua leo hii wilayani Itilima, mkoani Simiyu.
"Watumishi
wenzangu huu ni wakati wa kubadilika na kuona mwelekeo wa Serikali hii
ya awamu ya tano ukoje. Jukumu letu ni kuwatumikia Watanzania wote bila
kujali itikadi zao, rangi wala dini zao," alisisitiza.
Waziri
Mkuu aliwahakikishia watumishi hao kwamba Serikali inatambua changamoto
walizonazo kutokana na upya wa wilaya hiyo na mkoa huo na akawaahidi
kuwa itaboresha mazingira yenu.
"Msiwaadhibu
wananchi kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi zenu, tunajua
mnayo madai ya nauli, posho za mafunzo, kupandishwa madaraja na
malimbikizo ya likizo," alisema huku akishangiliwa.
Alisema
Serikali itayalipa madeni hayo japo haitamaliza yote kwa wakati mmoja
ila ana uhakika wa kukamilisha walau kwa asilimia 80.
Mapema,
akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Bibi Georgina
Bundala alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Machi 2012 na kupata
Halmashauri Julai 2013 haina kituo cha polisi cha wilaya, haina gereza,
Ofisi za TAKUKURU, mahakama ya wilaya wala benki.
Alisema wilaya hiyo haina hospitali ya wilaya ila akabainisha kuwa wamekwishatenga eneo la ekari 30 kwa ajili ya ujenzi huo.
"Pia tumekwishapima viwanja 123 na eneo la kujenga taasisi lenye ekari 143.8 limefanyiwa uthamini na fidia kukamilika," alisema
Chanzo>mpekuzi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MACHI 4, 2016.
0 comments:
Post a Comment