Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya
Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang ambaye amewasili hapa nchini jana
jioni tarehe 08 Machi, 2016 kwa ziara ya kiserikali ya siku nne,
amepokelewa rasmi na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika lango kuu lililopo Mashariki mwa
Ikulu, Rais Truong Tan Sang amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa
heshima yake na amepigiwa mizinga 21 iliyokwenda sambamba na nyimbo za
mataifa yote mawili.
Pamoja
na mapokezi hayo, Marais hao wawili wamefanya mazungumzo ya faragha
ambayo yamehudhuriwa pia na makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, na baadaye kufuatiwa na mazungumzo rasmi kati ya Rais Magufuli
na ujumbe wake na Rais Truong na Ujumbe wake.
Katika Mazungumzo hayo, Rais Magufuli
ameahidi kuuendeleza na kuuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati
ya Tanzania na Vietnam ambao ulijengwa na waasisi wa mataifa haya mawili
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Ho Chi Minh, hata
kabla ya Uhuru, huku akitilia mkazo juu ya ushirikiano katika maendeleo
ya kiuchumi.
Rais Magufuli amemweleza Rais Truong
Tan Sang kuwa katika miaka mitano ijayo, Tanzania imedhamiria kujikita
katika uanzishwaji wa viwanda vingi, na hivyo ametaka mahusiano kati ya
Tanzania na Vietnam yajielekeze katika kuendeleza Kilimo na ufugaji na
hivyo kuiwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula na pia kupata ziada
itakayouzwa nchi.
“Tunatambua jinsi Vietnam ilivyopiga
hatua kubwa katika uvuvi, uzalishaji wa kahawa na uzalishaji wa mpunga.
Uzalishaji katika maeneo hayo umeiwezesha kuwa nchi inayoongoza
duniani, na sisi Tanzania tunataka kujifunza kutoka kwenu” Amesisitiza Rais Magufuli.
Kufuatia hali hiyo, Rais Magufuli
amemuomba Rais Truong Tan Sang, kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya
nchi hizi mbili ujikite katika kuendeleza kilimo hususani kutumia zana
bora za kilimo badala ya jembe la mkono, Kilimo cha umwagiliaji badala
ya kutegemea mvua, kuzingatia mbinu bora za ugani, kukabiliana na wadudu
waharibifu wa mazao na kupata masoko ya mazao.
Kwa upande wake Rais wa Vietnam
Mheshimiwa Truong Tan Sang amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa
kuiongoza awamu ya Tano na amemhakikishia kuwa Vietnam itaendelea
kushirikiana na Tanzania, huku ikitambua mchango mkubwa uliotolewa na
watu wa Tanzania walioiunga mkono juhudi za kuiunganisha nchi hiyo na
kuwa Jamhuri ya Kisoshalisti mwaka 1968.
Amesema kwa kuzingatia mazingira bora
ya Tanzania yenye amani na utulivu, Vietnam imedhamiria kuwa Tanzania
iwe kituo chake cha kuzifikia nchi nyingine za Afrika Mashariki na
sehemu nyingine za Afrika.
Rais Truong Tan Sang ameomba mahusiano
ya Tanzania na Vietnam, sasa yajielekeze katika kuongeza Biashara, huku
akieleza kuwa biashara ya Dola za Marekani milioni takribani milioni 300
haitoshi, na hivyo amependekeza wafanyabiashara wa Tanzania
kuunganishwa na wenzao wa Vietnam ili mauzo ya bidhaa kutoka pande zote
mbili yaongezeke hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1 ifikapo mwaka
2020.
Ameongeza kuwa Vietnam ipo tayari
kutiliana saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano katika biashara,
Viwanda na Kilimo, na ametoa mwaliko kwa wakulima wa Tanzania kwenda
kujifunza nchini Vietnam.
Mara baada ya Mazungumzo hayo, Marais
wote wawili wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo
wote wawili wamesisitiza kuwa, nchi zao zipo tayari kukuza zaidi
mahusiano na ushirikiano kwa faida ya wananchi wake.
News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.
RELATED POSTS
MAMBO YA MSINGI RAIS MAGUFULI ALIYOMWELEZA RAIS WA VIETNAM JANA
Reviewed by Newspointtz
on
07:51:00
Rating: 5
0 comments:
Post a Comment