Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Abbas Tarimba amesema wapenzi wa mchezo wa pool table watalazimika kusubiri mpaka saa kumi ili kuweza kucheza mchezo huo.Watakaokiuka na kukutwa wanacheza kabla ya muda uliopangwa kutozwa faini isiyopungua Shilingi 300,000


Amesema atatoa mwongozo wa muda wa kuanza mchezo huo ambao utakuwa ni saa 10.00 jioni na kumaliza saa 5.00 usiku kwa siku za kazi, huku siku za mapumziko utaanza saa 8.00 mchana na kumalizika saa 6.00 usiku.

 Tarimba alisema Sheria ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), kifungu cha 52 katika kifungu kidogo cha kwanza sura ya 42, inaeleza asiye na kibali cha kuchezesha au atakayekiuka kanuni za mchezo huo, atashtakiwa na akikutwa na hatia atalazimika kulipa faini isiyopungua Sh300,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote viwili.

“Kila shughuli hapa nchini ina taratibu zake, watakaokiuka kwa kisingizio cha kuwa hiyo ndiyo ajira yao, watakaokutwa wanautumia mchezo huo kinyume cha sheria na kuugeuza kamari, watachukuliwa hatua za kinidhamu,”alisema.