Rais John Magufuli inaelekea amefuta utaratibu wa kupokea marais wenzake ulioonekana kutumiwa mara kadhaa na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete, na badala yake ameanza kufuata nyendo za wakuu wa mataifa kadhaa makubwa akiwamo Barack Obama wa Marekani.
Utaratibu unaoonekana kufutwa kwenye awamu hii ya Rais Magufuli ni ule wa kwenda kuwapokea marais wageni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kama ilivyozoeleka wakati wa Kikwete.
Wakati wa awamu yake ya urais, Kikwete alikuwa akienda uwanjani kuwasubiri marais waliokuwa wakiwasili nchini kwa ziara zilizokuwa na malengo mbalimbali.
Baada ya hapo Kikwete aliongozana na wageni wake hao katika msafara hadi Ikulu.
\Uchunguzi unaonyesha kuwa wakati wa ujio wa Rais wa Vietnam nchini, Truong Tan Sang, wiki hii umeonyesha kuwapo kwa mabadiliko makubwa katika protokali za kupokea marais.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ndiye aliyemuwakilisha Rais Magufuli kwenda kumpokea Sang.
Hata juzi, Rais huyo alipoondoka baada ya kumaliza ziara yake nchini, Majaliwa ndiye aliyemsindikiza kiongozi huyo kwenda uwanja wa ndege.
Utaratibu huo ni mpya katika protokali za mapokezi ya viongozi wakuu kama Truong, ambaye ni rais wa kwanza kutembelea nchi kwa ziara rasmi ya kiserikali tangu Magufuli aapishwe kuwa Rais Novemba 5, mwaka jana.
Rais Barack Obama wa Marekani amekuwa na utaratibu kama ulioanza
kutumiwa na Rais Magufuli ambapo wageni wa kitaifa wa Marekani hupokewa
na wasaidizi wake na yeye kuwasubiri Ikulu ya ‘White House’.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, marais wa kigeni ambao
wameshakanyaga ardhi ya Tanzania ni pamoja na Paul Kagame wa Rwanda,
Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya ambao walikutana
naye kwenye mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki
uliofanyika mkoani wa Arusha.
Alipoulizwa kuhusu utaratibu huo unaoonekana kuwa mpya wakati wa
mapokezi ya marais, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson
Msigwa, alikiri kwamba Rais huyo wa Vietnam alipokewa na Waziri Mkuu,
Majaliwa na kwamba hakuna tatizo katika hilo kwa sababu ni utaratibu wa
kawaida.
“Waziri Mkuu kwenda kumpokea Rais wa Vietnam uwanjani ilikuwa
sahihi kabisa kwa sabababu ni uamuzi tu nani aende,” alisema Msigwa.
“Mbona sisi tukienda kwao wakati mwingine Rais wetu anapokewa na Meya au
Mkuu wa Mkoa?
“Mapokezi ni mapokezi tu, kule uwanja wa ndege anaweza kwenda
yeyote kumpokea isipokuwa hapa Ikulu lazima Rais awepo mwenyewe
kumpokea.”
chanzo>mtembezi
0 comments:
Post a Comment