NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Rais Magufuli aipa MSD Hati Ya Kiwanja Chenya Ukubwa wa Hekari 5



RAIS Dk. John Magufuli kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametoa kiwanja chenye ukubwa wa ekari 5 kwa Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Luguluni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya ujenzi wa Bohari ya Dawa ili kuondoa upotevu wa fedha kwa maghala ya kukodi.

Ujenzi wa maghala katika kiwanja hicho utaokoa kiasi cha sh. bilioni 4 zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa ajili ya malipo ya maghala ya kukodi yaliyopo Mabibo Ubungo jijini pamoja na kanda mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa akikabidhi hati hiyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu Dar es Salaam jana mchana, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema, Rais ametoa ardhi hiyo ili kuepusha gharama zisizo na sababu kwa MSD.

Alisema agizo la rais fedha zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kukodi maghala hayo, zinapaswa kununua dawa ili kila Mtanzania apate huduma bora za kiafya.

“Rais aliniagiza niwape eneo, leo nimetekeleza agizo hilo kilichopo muanze ujenzi kama mlivyoomba kwa ajili ya kujenga ghala la dawa, naamini mtaanza mara moja balada ya kuendelea kukodi maghala na badala yake fedha zote zitumike kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba,” alisema Lukuvi na kuongeza;

“Kiwanja hiki ambacho kilikuwa cha Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kilichokuwa na ukubwa wa ekari 200, tumewapa ekari tano kama uhitaji wenu ulivyokuwa, nimewasamehe kodi ya premium na badala yake kiasi cha Sh16.7 hamtalipa na gharama mtakayotakiwa kulipa ni sh. milioni 2 pekee ili muanze ujenzi mara moja.”

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Bwanakunu alisema tayari wameshazungumza na Bodi ya wadhamini, Wizara ya Afya na wahisani hivyo ujenzi unatarajiwa kuanza mara moja Julai Mosi.

“Tunamshukuru sana Rais kwa sababu ombi hili limefanyiwa kazi kwa haraka sisi kama MSD tulishindwa kuhimili mikiki kutokana na gharama kubwa iliyokuwa ikielekezwa katika malipo ya ghala la kukodi pale ubungo mwaka wa fedha ulioisha tulilipa kiasi cha Sh3.5 bilioni na tukitarajia mwaka huu mpya wa fedha inafikia Sh4 bilioni kwa sababu ya malipo kwa dola,” alisema Bwanakunu.

Alisema katika eneo hilo jipya lililopo Luguluni wanatarajia kujenga zaidi ya maghala matano yenye ukubwa wa sikwea mita mita 5000 yatakayogharimu kiasi cha sh. bilioni 10 kila mojawapo, ujenzi huu utakapokamilika kanda zitakazonufaika ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro na Pwani na kuwa eneo hilo walilopata wanaweza kujenga kiwanda cha maji.
 
chanzo>mpekuzi
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment