NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Ripoti: Ushindi wa Trump ni hatari kwa dunia

Shirika moja la kimataifa limesema ushindi wa Donald Trump unachukuliwa kuwa miongoni mwa hatari 10 kuu zaidi zinazokabili dunia.

Shirika hilo la Economist Intelligence Unit linaonya kuwa iwapo Bw Trump atashinda urais Marekani, hilo huenda likavuruga uchumi wa dunia na kuongeza hatari za kisiasa na kiusalama dhidi ya Marekani.

Hata hivyo, shirika hilo halimtarajii Bw Trump, anayeongoza kwenye kinyang’anyiro cha kumchagua atakayepeperusha bendera ya chama cha Republican, kumshinda Bi Hillary Clinton ambaye shirika hilo linasema "ana uwezekano mkubwa sana kuwa mgombea wa chama cha Democratic".

Ushindi wa Trump unaorodheshwa kuwa hatari zaidi kwa dunia kushinda hata Uingereza kuondoka kutoka kwa Umoja wa Ulaya au hata makabiliano ya kivita katika bahari ya South China Sea.

Kuyumba kwa uchumi wa Uchina au Urusi kuingilia kivita Ukraine na Syria na kusababisha “vita baridi” vipya ni miongoni mwa mambo ambayo yanachukuliwa kuwa hatari zaidi ya ushindi wa Bw Trump.

"Kufikia sasa, Bw Trump ametoa maelezo machache sana kuhusu sera zake, na huwa anabadilisha sana msimamo wake,” EIU wanasema kwenye ripoti yao ya utathmini wa hatari zinazokabili dunia.
Utathmini huo huangazia pia athari za jambo fulani na uwezekano wa jambo hilo kutokea.
EIU hutumia kipimo cha moja hadi 25, na Bw Trump ana alama 12, sawa na hatari ya "kuongezeka kwa ugaidi wa kijihadi kuathiri uchumi wa dunia”.

"Amekuwa na msimamo mkali sana dhidi ya biashara huria, pamoja na Nafta, na ameituhumu Uchina mara nyingi kuwa taifa linalofanyia mchezo sarafu,” EIU inasema.

Shirika hilo limeonya kuwa matamshi yake makali dhidi ya Mexico na Uchina hasa yanaweza kusababisha vita vya kibiashara.

Bw Trump amependekeza ua ujengwe kati ya Marekani na Mexico kuzuia wahamiaji na pia ametetea kuuawa kwa jamaa za magaidi. Aidha, amependekeza kuvamiwa kwa Syria ili kuangamiza kundi la Islamic State.

EIU wanasema pendekezo msimamo wake kuhusu mzozo Mashariki ya Kati pamoja na pendekezo kwamba Waislamu wazuiwe kuingia Marekani vinaweza kutumiwa na makundi ya itikadi kali za Kiislamu kuwatafuta wafuasi zaidi.


chanzo>BBC
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment