Hatima
ya kesi ya Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka kupinga
kuilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zaidi ya Sh500 milioni kutoka
katika mgawo wa Sh1.62 bilioni zinazohusishwa na fedha zilizochotwa
Akaunti ya Tegeta Escrow, itajulikana Machi 29, wakati Bodi ya Rufaa za
Kodi (Trab) itakapotoa uamuzi.
Tarehe
hiyo imepangwa na Makamu Mwenyekiti wa Trab, Hakimu Agusta Mmbando
baada ya kukamilika kwa hatua ya usikilizwaji pande zote mbili kwenye
kesi hiyo.
Profesa
Tibaijuka alikata rufaa Trab baada ya TRA kumpelekea madai ya malipo ya
kodi ya Sh586 milioni kutokana na mgawo wa Sh1.62 bilioni anazodaiwa
kupokea kutokana na fedha zilizochotwa kutoka akaunti hiyo
iliyofunguliwa na Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni ya kufua nishati
hiyo ya IPTL kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya ununuzi wa umeme
wakati mzozo wao ukiwa mahakamani, lakini zikachotwa kwa njia ambayo
ilizua shaka.
Rufaa hiyo ilisikilizwa na Hakimu Mmbando Februari 17, 19 na 22 wakati Profesa Tibaijuka alipokuwa akitoa ushahidi.
Inadaiwa
kuwa Profesa Tibaijuka, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake wa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na sakata hilo,
aliwekewa fedha hizo kwenye akaunti yake na James Rugemalira, Mkurugenzi
wa VIP Engineering & Marketing Limited iliyokuwa kati ya wanahisa
wa IPTL.
Kutokana
na mgawo huo, Desemba 31, 2015, TRA ilimtaka alipe kodi hiyo, baada ya
kushindwa kufanya marejesho kutokana na mgawo huo.
Hata
hivyo, alipinga madai hayo na kisha akakata rufaa Trab kupinga hatua ya
TRA kumtaka alipe kiasi hicho cha kodi, pamoja na mambo mengine akidai
kuwa hajawahi kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira.
Katika
rufaa hiyo namba 22 ya mwaka 2015, Profesa Tibaijuka anadai kuwa
makadirio hayo ya TRA ya malipo ya kodi ni kinyume cha Sheria ya Kodi na
hakupaswa kufanya marejesho kwa kuwa hakupokea kipato chochote katika
muda huo uliotajwa.
Akiongozwa
na wakili wake, Dk Nshalla Rugemeleza wakati wa usikilizwaji wa shauri
hilo, Profesa Tibaijuka alidai kuwa fedha hizo zilikuwa ni mchango
uliotolewa kwa Taasisi ya Joha Trust, kwa ajili ya Shule ya Wasichana ya
Barbro Johansson inayomilikiwa na taasisi hiyo.
Profesa
Tibaijuka alidai kuwa yeye si mwanahisa wa taasisi hiyo, bali ni mmoja
wa wadhamini na kwamba TRA ilipuuza ushahidi wake kuwa VIP ilitoa
mchango kwa Joha Trust na yeye kama mdhamini alizipeleka Joha Trust
kupitia Bank M.
Aliongeza
kuwa TRA haikuzingatia ukweli kwamba Joha Trust na yeye ni vitu viwili
tofauti, huku akisisitiza kwamba fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya
Joha.
Hata
hivyo, wakili wa TRA, Noah Tito ilipinga madai ya Profesa Tibaijuka
akidai kuwa utetezi wake hauna msingi kwani fedha hizo ziliingia kwenye
akaunti binafsi ya Profesa Tibaijuka na siyo ya Joha Trust.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment