newswpointtz.blog
Waziri wa Ardhi, William Lukuvi amesema rushwa imekithiri kwenye sekta ya ardhi kiasi kwamba wafanyabiashara wawili walimuahidi rushwa ya Sh5 bilioni afanikishe mpango wao wa kuiuzia Serikali ardhi kwenye eneo linalotakiwa kujengwa mji wa kisasa wa Kigamboni.
Mji
huo kabambe wa Kigamboni unajumuisha kata za Kigamboni, Tungi,
Vijibweni, Mjimwema, Kibada, Somangila na eneo lote lina ukubwa wa
takribani ekari 6,000.
Awali
mradi huo ulitarajiwa kugharimu Sh13 trilioni ambazo zingetolewa na
Serikali, lakini ikaamua kushirikisha sekta binafsi ili zishiriki
kuujenga na Serikali ishughulikie uwezeshaji wa awali.
Lukuvi,
ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa takriban miaka
mitano kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka jana na
kubakizwa wizara hiyo na Rais John Magufuli, alitoa siri hiyo mwishoni
mwa wiki iliyopita.
Mbunge
huyo wa miaka mingi wa Isimani mkoani Iringa alisema amegundua kuna
mtandao mkubwa wa rushwa unaoanzia ngazi ya halmashauri mpaka wizarani
ambao unahusisha maofisa wa Serikali na viongozi wa wizara.
Waziri
Lukuvi alisema mtandao huo ni hatari na unaweza kusababisha mtu
ashindwe kufanya kazi ya wananchi iwapo ataendekeza rushwa.
“Hapa (Wizara ya Ardhi) fedha ipo,” alisema Lukuvi ambaye amekuwa mbunge wa Isimani tangu mwaka 1995.
“Kama
ukiwa na tamaa huwezi fanya kazi uliyotumwa. Kuna wakati walikuja
wafanyabiashara wawili wakubwa na kutaka wanipe Sh5 bilioni ili nikubali
kupitisha mradi wao wa mabilioni ya shilingi na walitangaza kwa
marafiki zangu kuwa wangenipa fedha, lakini hapa hawawezi” alisema Lukuvi.
“Wakati
naingia tu wizara hii, nilikuta harakati za kukamilisha mradi wa
Kigamboni ukiwa katika hatua za mwisho na kila kitu kilikuwa
kimekamilika. Lakini nilipopitia vizuri, nilikataa kuwalipa
wafanyabiashara hao. Cha ajabu hazikupita siku mbili wafanyabiashara hao
walipata taarifa wakaja mbio kutaka kuniona.”
Kwa
mujibu wa Waziri Lukuvi, wafanyabiashara hao walitaka walipwe kiasi cha
Sh141 milioni kwa kila ekari wakati wao walinunua ardhi kutoka kwa
wananchi kwa Sh5 milioni kwa ekari, jambo ambalo alisema lilishapitishwa
awali.
“Niligundua
pale kuna udanganyifu na wizi mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue
kutoka kwa wananchi ekari moja kwa Sh5 milioni, kisha Serikali tumlipe
Sh141 milioni kwa ekari kwa kuvuka pantoni tu. Ni wizi mkubwa. Kama
kweli Serikali ina fedha hizo kwa nini tusimlipe mwananchi moja kwa
moja?” alihoji.
Waziri
Lukuvi alisema endapo njama hizo zingefanikiwa, Serikali ingetumia
zaidi ya Sh84 bilioni kuwalipa wawekezaji hao hewa kwa kuwa mmoja
anamiliki takribani ekari 200 na mwingine 400.
“Niliwaambia
Serikali haiwezi kuwalipa fedha hizo na badala yake waende kuiendeleza
ardhi wenyewe kulingana na mradi unavyotaka. Walitaka kutajirika kwa
ujanja ujanja,” alisema Lukuvi.
“Eti
walidai wamekopa benki kwa ajili ya mradi huo. Haiingii akilini mtu
utumie Sh5 milioni, halafu uje uvune mabilioni ya fedha kwa kuvuka
pantoni tu.”
Hata hivyo, Lukuvi alikataa kutaja majina ya wafanyabiashara hao.
Akiongea
na gazeti moja la kila wiki mwaka 2013, Profesa Anna Tibaijuka, waziri
aliyemtangulia Lukuvi kwenye wizara hiyo, alisema tayari kampuni mbili
za Miworld kutoka Dubai na China Hope (China) zilishasaini mkataba wa
maridhiano na Serikali wa kujenga nyumba takriban 20,900 kwenye eneo
hilo.
Miworld
ilisaini mkataba wa kujenga nyumba 5,000 wakati China Hope ilitaka
kujenga nyumba 15,900 kwenye eneo hilo la mradi wa mji mpya.
Profesa Tibaijuka aliliambia gazeti hilo wakati huo kuwa wananchi wangefidiwa kwa bei za soko kwa mujibu wa sheria, akisema ekari moja ingefidiwa Sh141 milioni kwa ajili ya kumuwezesha kulipia gharama ya nyumba mpya mbadala.
Akizungumzia
migogoro ya ardhi, Waziri Lukuvi alisema amegundua mingi inasababishwa
na maofisa na viongozi wa wizara hiyo wasio waaminifu, lakini pia
wawekezaji wenye tamaa ya kumiliki kiasi kikubwa cha ardhi hata kama
hawana shughuli nayo.
“Nimegundua
kuna watu hapa wanataka kumiliki ardhi kila sehemu. (Mtu huyo) Atafanya
kila njia ashirikiane na watumishi wasio waaminifu ili wampatie eneo
hata kama limeshauzwa,” aliongeza.
Lukuvi
alisema wengi wao ni wafanyabiashara wenye asili ya Kiarabu na Asia
ambao kwa muda aliokaa wizarani hapo amegundua wamehodhi mashamba
katika miradi yote ya viwanja au mashamba iwe ya halmashauri au wizara.
“Wanasiasa
na viongozi wa Serikali wanaohodhi maeneo wapo, lakini siyo wengi
ukilinganisha na hawa wafanyabiashara wengi wenye tamaa ambao
wakishapata ardhi wanatumia kukopa mabilioni ya fedha ndani na nje ya
nchi kisha wanawekeza katika miradi yao mingine ikiwamo kujenga majumba
katika nchi za Dubai na Ulaya na kuyatelekeza maeneo hayo kuwa mapori
hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wasio na maeneo."
Akizungumzia
matarajio yake, Waziri Lukuvi alisema endapo Rais John Magufuli
ataendelea kumuweka katika wizara hiyo anatamani amalize migogoro yote
baina ya wananchi katika kipindi cha miaka mitano
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment