Mkazi
wa kijiji cha Kanyama Kata ya Bujora Wilaya ya Magu mkoani Mwanza,
Erick Mkundi (23), ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya kazi kama
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kongoro akiwa hana sifa hiyo.
Mtuhumiwa
huyo anadaiwa kuifanya kazi hiyo kuanzia Januari hadi Aprili 6, mwaka
huu alipobainika baada ya kushindwa kujitambulisha kwa Hakimu Mfawidhi
wa wilaya hiyo, Edmund Kente, kuwa ni hakimu na bila kuonyesha nyaraka
zozote zinazomthibitisha kuwa na taaluma hiyo.
Aidha,
ilidaiwa kuwa Mkundi alijikabidhi katika mahakama hiyo na kuanza
kuendesha kesi na hadi anatiwa mbaroni, tayari alishatoa hukumu kwa
washtakiwa wanne na wengine kadhaa kuwasotesha mahabusu.
Akizungumza
jana, mmoja wa watumishi wa mahakama hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe
kwa madai kuwa si msemaji, alieleza kuwa walifanya kazi na Mkundi kwa
miezi minne wakiamini kwamba ni mtumishi halali wa Idara ya Mahakama.
“Mkundi
tuliamini ni hakimu halali, kwani alikuwa akiletwa na gari kama
mheshimiwa fulani hivi, lakini baada ya kukamatwa Aprili 7, mwaka huu,
ndipo tulipogundua ni mfanyakazi ‘hewa’, alisema mtoa taarifa huyo.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Magu, Charles
Mkapa, alisema Mkundi alikamatwa baada ya polisi kupewa taarifa zake za
kufanya kazi bila kibali.
“Kweli
tunamshikilia Mkundi tangu Aprili 7, mwaka huu, kwa tuhuma hizo, lakini
taarifa kamili mnaweza kuzipata kwa Hakimu wa Wilaya ya Magu, kazi yetu
ilikuwa kumtia mikononi mwa polisi,” alisema Kamanda Mkapa.
Awali,
ilisemekana mtuhumiwa huyo aligundulika kuwa ‘feki’ baada ya kushindwa
kulipa Sh. 40,000 yakiwa ni malipo ya gari alilokodi kwa ajili ya
kutembelea kwenda na kurudi kazini pamoja na maeneo mbalimbali.
Habari
zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa Mkundi baada ya kushindwa kulipa gharama
hizo, mmiliki wa gari alitoa taarifa kwa bosi wake wilayani na ndipo
alipoanza kufuatiliwa.
Aidha,
Mkundi ilidaiwa alikuwa akipokea rushwa na zawadi mbalimbali kutoka kwa
watu aliokuwa akiwahudumia kimahakama, zikiwamo mbuzi pamoja na fedha
kwa lengo la kusimamia kwa ukaribu tuhuma zinazowakabili.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe, alipoulizwa
kuhusiana na tukio la ‘hakimu huyo feki’, alisema hajapata taarifa
kamili, lakini atalizungumzia suala hilo leo.
0 comments:
Post a Comment