NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Kamishna,Dk Shein unafiki si msosi wa kula

         zombi
Watu waliofunika nyuso wakiwa na silaha za moto na jadi, katika gari KM 155 yaserekali, wakipita maeneno ya Kilimani mjini Zanzibar, Alhamis tarehe 4, Febuari mwaka huu.
“Serekali zote mbili hazitomvumilia mtu yeyote au kikundi cha watu watakaojaribu kuichezea amani na utulivu wetu uliopo”.

Pigia mstari maneno hayo kutoka kwa, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Muhammed, alipoyasema Alkhamisi ya tarehe 24 Machi, wakati wa Sherehe ya kuapishwa kwake katika uwanja wa Amani mjini Unguja.

Alkhamisi ya tarekhe 4, Febuari mwaka huu, watu waliofunika nyuso zao wakiwa na silaha za jadi na moto, walipita katika maeneo ya Kilimani mjini Zanzibar, wakiwa katika gari lenye namba za usajili KM 155.

KM ni kifupi cha KMKM-Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo. Ufupi ni kuwa ni gari la kikosi cha Serekali ya Mapinduzi Zanzibar, kinacholinda rasilimali za Zanzibar kupitia ardhini na nchi kavu.
Mchana kweupe Alkhamisi ya siku hiyo ambayo wafunika nyuso hao walionekana (Mazombi) , hadi kufika jioni walikuwa tayari wameshaharibu na kujeruhi watu.

Kuna masuali ya kujiuliza hapa: Kuna watu wowote wamekamatwa kwa tuhuma za kupita mitaani na silaha za moto na jadi, wakiwa na magari ya vikosi vya serekali wakipiga watu na kuharibu?
Dk Shein anazungumzia vikundi vipi vya watu?

 Kama hakuna Zombi hata moja lililokamatwa hadi sasa, ni kikundi gani cha watu ambacho kinaharibu amani na utulivu wa Zanzibar, kama si Mazombi?

Anakusudia kutomvumilia nani kama watu wake kutoka katika vikosi vyake ndio wanafanya fujo la wala hawakamatwi! Ama vikundi avikusudiavyo ni wapinzani wake kisiasa? Pengine ukiwa mpinzani ndio unachezea.

Wiki moja nyuma baada ya nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame kutupiwa bomu ndani, Kamishna Hamdani akaamua kuwakusanya waandishi wa habari na kutoa maneno ya ajabu sana.

Kamishna anashangaa kwa kusema, “Kama kweli kamishna anaripuliwa, hivi atabakishwa nan?”.
Wakati anauliza sulai hili pia Kamishana alipaswa kuulizwa, kwani Mazombie wamembakisha nani? Kamishna anaona ajabu mno, ni hatari kwamba nyumba yake imeshambuliwa, lakini jinsi Mazombi walivyogaragara watu, hakuna ajabu wala si hatari kwake.

Anaendelea kwa kusema; “Hatuwezi tukaacha hiyo hali katika mazingira hayo, tusaidieni kuwambia wananchi ukweli, kwamba kilichofanyika si halali, na hatukivumilii, (huku akigonga mimbari)”.
Ni kweli kilichofanywa si halali, hakivumiliki lakini mbona wananchi wakipigwa huji na maneno kama haya, mbona wananchi wakipigwa hupandwi na hasira ukawa unagonga meza. Kamishna umepandwa na hasira kwa sababu nyumba yako ndio imetupiwa bomu?

Hukupandwa na hasira kwa Wazanzibari waliocharzwa bakora na vipigo?

Anasema :“tunaanza kazi sasa, anayesema aseme, anayenuna anune, lakini hili lazima likome, lazima likome” .

Mbona kama kuanza kazi ilihitajika ianze tangu Mazombi walipoanza kupiga virungu, risasi na kuharibu, kwanini kazi ianze kwa kuwa Kamishna katupiwa bomu.
Hivi ni kusema kuwa maisha ya Kamishna yanathamini sana kuliko ya Wazanzibari wengine? Watu wamepigwa lakini hakutangaza kuanza kazi, katangaza baad aya nyumba yake kutupiwa bomu.

Nimalize kumnukuu aliposema ; “Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama, vimeamua kuongeza nguvu ya ulinzi katika maeneo yote ya nchi kwa kufanya doria, kuongeza kasi za ukusanyaji wa taarifa za kiitelejinsia, na kufanya misako katika maeneo yanayotiliwa shaka, ya kupangwa vitendo vya kihalifu na vitendo vinavyoleta khofu kwa jamii”.

Kwanini uongeze nguvu leo? Leo! Kwanini leo Kamishna, eti kwakuwa bomu nyumbani pako, taarifa za kintelejensia zilihitajika zikusanywe zamani kuwajua Mazombi ni akina nani kwa majina yao, pia kufanya msako huko katika vikosi ambako wanatoka, magari wanayopewa na silaha, pia mungeanza kufanya msako na kuwashika Mazombi ambao wanatembea mchana kweupe wakifanya uhalifu na kutia khofu watu.

Huu ni unafiki, anayoyasema Kamishna yalihitajika kufanyika zamani sio muda huu kwakuwa eti kuna mripuko nyumbani kwake, Wazanzibari wameanza kupigwa na Mazombi zamani, na wala hakujitokeza na kupiga meza kwa hasira akiahidi kuwakamata, lugha ya ukali na hatua madhubuti inakuja kwa kuwa paa la nyumba yake limeizuka kwa mripuko.

Baada ya bomu kutupwa kila kona askari walimwagwa kama tuko Mogadishu vile, sababu nikuwa nyumba ya Kamishna imetupiwa bomu, lakini wavaa soksi wakipiga, kuharibu, kujeruhi, huoni askari wakimwagwa kuwatafuta.

Polisi wakiulizwa wanasema; “wahuni tu”, wahuni wanawezaje kuwa na magari ya KVZ na KM? Wahuni gani hao wenye silaha za moto na wavaa magwanda ya vikosi vya serekali?
Siku chahce baada maeneo ya Mpendae- Unguja watu 30 walikamatwa na Polisi na kupelekwa kituo cha polisi Madema baadhi yao wamepigwa vibaya na mabomu ya machozi yalirushwa na njia zikafungwa, hadi sasa ni zaidi ya watu 40 wameshakamatwa wengi wameshaachiliwa.

Madhila yote hayo ni kwakuwa kibanda cha kamisha kimetupiwa bomu, sasa uliza Mazombi
 walipopiga na kutesa, kujeruhi, kuna mtu yoyote hadi muda huu kakamatwa kwa angalau tuhuma? Kuna askari ambao walimwagwa mitaani kuwatafuta Mazombi?
Anachokihubiri Dk Shein katika sherehe za kuapishwa kwake, hakina mantiki yoyote ikiwa makundi ya wachafua amani yapo Zanzibar, yanatumia gari za vikosi vya serekali na silaha na hayachukuliwi hatua yoyote.

Haiyeleweki ni wachafua amani gani kama si Mazombi ambao Dk Shein anawakusudiwa, inaonekana kumbe Mazombi sio kabisa anaowaongelea kwa sababu hawashikwi wala hawafuatiliwi.
Huu unaooneshwa na Dk Shein na Kamishna wake ni unafiki, wanajua wazi kinachoendelea na wanawajua fika wanaochafua amani ya Zanzibar kwa kupita kupiga watu na kuharibu.
Porojo wanazozitoa wakiwa mbele ya kamera hazina maana yoyote, kama kweli wanajali amani ya Zanzibar wangekwenda kuikamata gari ya KM 155 kisha wakawakamata walioitumia mchana wa tarehe 4 Febuari.

Lakini hilo halijafanyika, Mazombi wapo na wanadunda na kila siku wanajitokeza kupiga na kuondoka. Dk Shein na Kamishna kwao mchafua amani ni yule ambaye haungi mkono CCM. Wanakula msosi wa unafiki na kuwalisha wengine kwa maslahi yao.
Ni uongo na unafiki wanaouzungumza mbele ya vyombo vya habari kwa sababu ukweli wanaujua na wala hawataki kuusema, ni watu wazima lakini wanafiki, waongo.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment