NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Mahakama yakataa CD ya Askofu Gwajima kudaiwa kumtusi Askofu Pengo



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali ombi la Jamhuri la kupokea CD pamoja na picha kama kielelezo katika kesi inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, akidaiwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama pengo.

Uamuzi huo ulisomwa jana mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.

Katika ombi lake, upande wa Jamhuri ulikuwa ukiitaka mahakama hiyo ipokee CD ya siku ya tukio hilo, huku upande wa utetezi ukipinga kupokelewa kwa CD hiyo.

Hakimu Mkeha alisema mahakama imetupilia mbali ombi la kupokea kielelezo hicho kwa kuwa upande wa Jamhuri umeshindwa kutimiza vigezo vya kisheria cha kuwasilisha vilelezo vya eletroniki mahakamani.

Awali, wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alipinga kupokelewa kwa CD hiyo kwa madai kwamba shahidi aliyekuwa anawasilisha hakustahili kwani siye aliyeitengeneza CD hiyo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, akijibu hoja hiyo, alidai shahidi huyo ni mtaalam wa vielelezo vya elektoniki na picha na ndiye aliyeifanyia uchunguzi CD hiyo.
 
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Mei 4 mwaka huu.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment