BUNGE limetoa siku tatu kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mkataba wa Kampuni Lugumi Enterprises wenye thamani ya Sh bilioni 37.
Hatua
hii inakuja siku mbili baada ya jeshi hilo kudaiwa kukaidi agizo la
kamati hiyo, iliyotaka likabidhi nyaraka za utekelezaji wa mkataba
ufanyiwe tathmini kutokana na malalamiko yaliyotolewa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) katika hesabu za mwaka 2013/2014.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshi Hilaly
alisema agizo la kamati la kutaka mkataba huo, lilitolewa wiki iliyopita
kuwezesha wabunge kuangalia utekelezaji wake.
“Jana
(juzi) ilikuwa siku ya mwisho kwa jeshi kuwasilisha mkataba huo ofisi
za Bunge, lakini mpaka leo (jana) muda huu ninapozungumza nanyi (saa
7:30 mchana) walikuwa hawajawasilisha. “
"Siku
zote tumekuwa tukitoa maagizo kwa mdomo na taasisi nyingi zimekuwa
zikitekeleza, lakini hili la mkataba wa Lugumi naona kwa wenzetu
limekuwa gumu, hivyo tumeamua kuwakumbusha kwa maandishi,” alisema.
Alisema
kamati hiyo imetoa siku tatu tangu barua itakapopelekwa na ofisi za
Bunge, kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kamati hiyo iweze kupitia
utekelezaji wa mkataba huo na baadaye kupeleka mapendekezo kwenye
Bunge.
“
Katika suala hili, Kamati haitarudi nyuma, hivyo tunawaomba wenzetu wa
Jeshi la Polisi kutupa ushirikiano, si jambo la peke yangu kuamua, ni la
Bunge, baada ya kupitia tunapeleka mapendekezo bungeni ambalo ndilo
litakaloamua nini kifanyike,” alisisitiza.
Kamati ya PAC ilipokuwa ikipitia hesabu za Jeshi la Polisi, ilibaini kuwapo mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises .
Kupitia
mkataba huo wa mwaka 2011, Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa zabuni
ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi
108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Inadaiwa
kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37 ikiwa
ni sawa na asilimia 99 ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine katika
vituo 14 pekee katika jiji la Dar es Salaam, ambavyo pia inadaiwa
havijulikani maeneo vilipo.
0 comments:
Post a Comment