Watu watano wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa, baada ya
nyumba waliyokuwa wakiishi kuangukiwa na kifusi na mti wakiwa wamelala,
ajali hiyo ilisababishwa na kupasuka kwa karo la majitaka la nyumba ya
jirani iliyo juu ya mlima.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Christopher Fuime alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa karo
hilo na kwamba maji yaliyotoka kwa kasi yaling’oa mti, kifusi na kisha
kuifunika nyumba ya jirani iliyojengwa bondeni na kusababisha vifo
hivyo.
Alisema tukio hilo lilitokea jana alfajiri katika Mtaa wa
Ukwamani Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam, na waliokufa ni Ephraim
Manguli (47), watoto wake Daniel Ephraim (5) na Frederick Ephraim (1).
Wengine ni mjukuu wa mwenye nyumba hiyo, Greyson Clarence (3) pamoja na
msichana wa kazi za ndani aliyetambulika kwa jina moja la Maria.
“Majeruhi
ni pamoja na Emilia Nakiete (19) aliyejeruhiwa mkono wa kulia na kidevu
na Fadhili Fariji (8) aliyejeruhiwa mguu wa kulia. Wengine watatu
walitibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kuruhusiwa. Majeruhi
wawili bado wamelazwa na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitalini
hapo,” alisema Kamanda Fuime.
Baada ya kutafutwa, mmiliki wa
nyumba hiyo Blandina Clarence Akilizao (49), alisema nyumba yake ilikuwa
na wapangaji sita wenye familia, huku familia yake ikiwa na watu saba.
“Ndani
ya nyumba nilikuwa na watoto wawili, wadogo zangu wawili na wajukuu
wawili, pia kulikuwa na familia tano zilizokuwa na watu 17 jumla,”
alisema mama huyo kwa uchungu.
Blandina alisema nyumba hiyo
aliachiwa na mumewe aliyefariki dunia mwaka 2000 na kwamba hivi sasa
hana msaada wowote, kwani akiba ya fedha aliyokuwa nayo kiasi cha
Sh200,000 imefukiwa na kifusi na hajui namna ya kuipata.
Mmoja
wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mpangaji, Msafiri Nyamolelo alisema
ajali hiyo ilitokea ghafla na kabla ya ukuta kuanguka, ulisikika
mlipuko na baadaye kelele za maji, kisha kishindo kikubwa juu ya paa.
“Karo
lilipasuka na kwa kuwa ardhi hiyo hapo juu kwa muda mrefu ni dampo
lenye mifuko mingi, ardhi ilikuwa imeoza, hivyo miti mikubwa ambayo
iliota huko iling’oka baada ya karo kupasuka na kutua juu ya paa la
nyumba sambamba na udongo kutoka juu nao ukafunika,” alisimulia
Nyamolelo.
Akizungumzia tukio hilo, Katibu Mtendaji wa Mtaa wa
Ukwamani, Kata ya Kawe Kassim Mbezi alisema chanzo cha ajali ni kupasuka
kwa karo la choo na maji yaliyomwagika ambayo yaliuzoa mti huo na
kifusi kilisombwa na kuifunika nyumba hiyo.
“Tulipofika eneo la
tukio tuliwakimbiza majeruhi wote Mwananyamala, lakini kwa bahati mbaya
walifariki baada ya kufika mapokezi wote walitoka wakiwa bado wanahema,
lakini ilipofika saa tatu asubuhi tukaambiwa kwamba kulikuwa na ‘house
girl’ hivyo baada ya kufukuafukua tukaupata mkono na baadaye kuufikia
mwili mzima, huyu tulimtoa akiwa tayari amefariki,” alisema Mbezi.
Mbezi
alitoa wito kwa wakazi wa bonde hilo kuhama kwa kuwa gema bado
linaonekana na ni hatari na changamoto kubwa ni namna ya kukabiliana na
maafa kabla ya kutokea.
0 comments:
Post a Comment