CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimelaani vikali tabia ya baadhi ya watu
wanaotumia vibaya jina la Chama hicho kuwatapeli wananchi kutoa fedha
ili wapatiwe nafasi za ajira katika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
jambo ambalo sio sahihi.
Kimewataka
wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kuacha tabia ya
kuwaaminisha watu kwamba CCM inatoa nafasi mbali mbali za ajira kwani
kufanya hivyo ni kuwagombanisha viongozi na wananchi wao.
Akitoa
taarifa kwa Vyombo vya Habari, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu
Vuai Ali Vuai alisema Chama hicho hakihusiki na utoaji wa ajira ya aina
yoyote, hivyo watu wanasambaza utapeli huo kwa njia ya simu na mitandao
ya kijamii lengo lao ni kuchafua taswira njema ya chama hicho.
Akifafanua
zaidi Ndugu Vuai amesema suala la ajira katika taasisi za kiserikali na
binafsi zinazolewa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa hasa baada ya
kutolewa matangazo maalum kulinga na nafasi za ajira zilizopo na sio
kutumia simu za mkononi kuwapigia watu ili waweze kutoa fedha kwa ajili
ya kuwapatiwa ajira hizo.
“Nimepigiwa
simu nyingi na baadhi ya watu wangu wa karibu wakiniuliza juu ya
taarifa za Chama kuuza nafasi za ajira, taarifa ambazo nimezipokea kwa
mshangao mkubwa kwani ndani ya chama chetu hakuna utaratibu huo.
Nawataka wananchi kuwa macho na makini na matapeli wanaotumia hila
tofauti kuwaadaa watu kwa nia ya kujipatia fedha kwa njia za
udanganyifu” Alisisitiza Vuai.
Naibu
Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar, alitoa wito kwa wananchi kuwa makini
na matapeli hao na mtu yeyote atakayepigiwa simu na kuambiwa atoe kima
chochote cha fedha kwa lengo la kupatiwa ajira na CCM asikubali kufanya
hivyo na badala yake atoe taarifa haraka katika vyombo vya dola, ili
sheria ichuke mkondo wake.
Aliwasihi
wananchi kuendelea kuamini kwamba CCM ni Chama kilichokomaa kisiasa na
uzoefu mkubwa wa kusimamia demokrasia ya kweli, usawa, haki, utawala
bora, a hivyo hakiwezi kujihusisha na vitendo viovu kwa jamii.
Naibu
Katibu Mkuu wa CCM alisisitiza kuwa suala la ajira za JWTZ, Idara
Maalum za SMZ na zile za Taasisi nyengine za seriikali, zote hizo
zinatolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa na Baraza la
Wawakilishi Zanzibar (BLW).
Alisema
kuwa haiwezekani hata kidogo Chama hicho (CCM) kitowe ajira na kuongeza
kuwa taarifa hizo zinazosambazwa na watu ni za kitapeli na zinalenga
kuchafua jina la Naibu Katibu Mkuu huyo pamoja na CCM kwa jumla.
Aliwaomba
wananchi wazipuuze taarifa hizo na wawe macho na utapeli wa aina hiyo
uliozagaa Zanzibar na maeneo mengine nchini, kwani unafanywa na wapinga
maendeleo ya CCM na Taifa kwa jumla.
0 comments:
Post a Comment