NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Chadema Wamtaka Rais Magufuli Amfuate Lowassa Ili Amshauri Kuhusu Sukari

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Rais John Magufuli kuweka siasa kando na kuomba ushauri kwa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ili kutatua tatizo la kuadimika kwa sukari.

Kauli hiyo ilitolewa na naibu katibu mkuu wa Chadema, Salim Mwalimu juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Moto wilayani Monduli Mkoa wa Arusha ambako Lowassa alizungumza na wananchi kuwashukuru kwa kumpigia kura na akatangaza mpango wa kuzunguka nchi nzima kwa lengo hilo.

Tangu Rais atangaze kudhibiti uagizaji sukari kutoka nje na baadaye Bodi ya Sukari kutangaza bei elekezi, bidhaa hiyo muhimu imepanda bei kutoka Sh1,800 hadi kufikia Sh5,000 kwa kilo na kwa sasa imeadimika madukani, wakati Serikali ikisaka wafanyabiashara inaowatuhumu kuwa wameificha kwenye maghala kwa lengo la kuihujumu.

Akizungumza kabla ya kumruhusu Lowassa kuongea na wananchi hao, Mwalimu alisema inaonekana tatizo la sukari linaelekea kuishinda Serikali na hivyo inahitaji msaada wa ushauri.

“Tatizo la sukari kalianzisha yeye mwenyewe Magufuli na sasa anashindwa kulitatua,” alisema Mwalimu na kuongeza:

“Mtu pekee atakayemsaidia ni Lowassa. Huyu alijipanga na alijiandaa kuongoza nchi.”

Mwalimu alisema Lowassa amevumilia mengi kwa kuwa amenyanyaswa, ameonewa na kusimangwa lakini hakujibu.

“Amepitia kipimo cha mwisho cha utu, ni cha mwisho. Walimuonea mchana kweupe akavumilia. Walimsimanga mchana kweupe mpaka watoto wadogo walikuwa wakimuona Lowassa kama vile saizi yao, akavumilia,” alisema Mwalimu.

“Ninajua vijana waliumia, mzee. Lakini leo warudi nyuma wafikirie maisha yao. Ni nani angetoka nyumbani kwa kauli moja ya Lowassa, kumshika mtoto wake mkono kumpeleka shule kama Lowassa angeangalia ushetani na kumuacha Mungu,” alisema akirejea kauli ya Lowassa kuwa alikuwa akipigiwa simu na watu kumtaka atoe kauli baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana kutangazwa, lakini akaawaambia watulie.

Lowassa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema baada ya kuenguliwa CCM, alishika nafasi ya pili kwenye mbio hizo akipata kura milioni 6.07 idadi ambayo ni rekodi kwa mgombea wa upinzani tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992. Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura milioni 8.8.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Lowassa aliwataka wananchi kuendelea kutulia, akisema mwaka 2020 hauko mbali na Chadema inaendelea kujipanga upya ili kuhakikisha inashika dola na kuondoa kero zao.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Chadema kutoka makao makuu, mkoa pamoja na makada waliojiunga wakitokea CCM wa wilaya ya Monduli, Lowassa alisema wafuasi wa ukawa wajiandae kwa mikutano hiyo.

Huku akishangiliwa na wananchi hao waliokuwa wakimkatisha kwa kelele za shangwe, Lowassa alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake wamejipanga kufanya ziara ya kuijenga Chadema nchi nzima.

“Nina hakika tumewashika pabaya CCM na tumewaumiza sana. Sasa kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tutazunguka nchi nzima tunataka kuiweka Chadema kwenye chama cha siasa na si uanaharakati,” alisema.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba 25 mwaka jana, Lowassa aliwashukuru wananchi kwa kumpa kura nyingi akisema hata walioiba kura zake wanajua na dunia inajua kuwa alishinda.

“Niliamua kukaa kimya kwani najua ningesema jambo moja nchi yetu ingeangamia. Na vijana kila kona ya nchi walikuwa wakinipigia simu wakidai wanasubiri neno kutoka kwangu,” alisema.

“Sikufurahishwa na kwenda Ikulu kwa mikono iliyojaa damu. Kuna siku nitakwenda Ikulu kwa mikono safi ya Watanzania, nina hakika na rafiki zetu wanajua kabisa kwamba hawakushinda.”
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment