NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Madaktari Wataka Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) Itumbuliwe


Waganga wafawidhi wa Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, wamesema Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) ni “jipu” linalohitaji kutumbuliwa kutokana na kuwa na mfumo usioridhisha wa utoaji huduma za dawa.

Wakizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, madaktari hao walisema MSD inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa ya utendaji kazi wake, kama siyo kutumbuliwa kutokana na kuwafanya wafanye kazi katika mazingira magumu na yasiyo na dawa.

Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Azizi Msuya alisema changamoto iliyopo ni upatikanaji wa dawa na mara nyingi wanachoomba MSD sicho wanachopata na kinawaletea uhasama na chuki kwa wagonjwa.

“Wao wananunua palepale na sisi tungeruhusiwa tungenunua. Maduka kama Salama, kopo moja la dawa aina ya paracetamol ni Sh7,000, lakini tukinunua kwao inakuwa Sh15,000 la sivyo turuhusiwe kununua wenyewe kuliko kusubiri dawa mwezi mzima,” alisema Msuya.

Alisema unaweza kuomba dawa aina nyingi zikiwamo za kuponya maisha haraka kama za kuzuia damu kutoka, kuzuia kifua kubana, ukapata nyingine hizo ukakosa. Hivyo kuna hatari ya kufiwa na mgonjwa mkononi.

Dk Emmanuel Kombe, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makongo alisema Serikali inapeleka fedha na vituo vina fedha yake, lakini cha kushangaza utata wa kupatikana mahitaji yaliyoagizwa kila siku upo palepale.

“Wauguzi wanatukanwa, wanakuwa maadui wa wananchi kwa sababu hospitali hazina dawa, hakuna mwananchi anayefahamu kama MSD ndiyo hawajaleta,” alisema Kombe.

Dk Sebastian Mapunda Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kigogo alisema hiyo ni changamoto ya muda mrefu na wao kama watendaji wanaoshughulika na wagonjwa inawapa shida.

Alisema wananchi wanapoona dawa katika maduka binafsi halafu hospitali hakuna, wanaona kama kuna mchezo unafanywa, kumbe MSD wapo kati kukwamisha.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alisema atamwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amuombe Rais atumbue jipu la MSD.

Tangu aapishwe kuwa Mkuu wa Wilaya, hiyo ndiyo taasisi ya kwanza kukutana nayo na kusikiliza kero zao.

Alisema ameanza na afya kwa sababu ndiyo sekta yenye changamoto nyingi ikiwamo hiyo ya dawa. Hivyo atalishughulikia suala hilo kwa kila njia ikiwamo kumshirikisha Mkuu wa Mkoa.

“Haiwezekani fedha ipo dawa hakuna na hakuna jibu la msingi, na haiwezekani dawa kusubiri taratibu mwezi mzima, wiki tatu kama hakuna ielezwe hakuna ili ufanyike utaratibu wa kununua zinakopatikana kwa sababu afya za binadamu hazitambui Sheria za Ununuzi,” alisema Hapi.

Ofisa Habari wa (MSD), Eti Kusiluka alipingana na madai hayo akieleza kuwa hakuna utaratibu wa kupokea fedha wanapoagiza dawa zaidi ya kupokea mahitaji ya wateja wao na kuyafanyia kazi.

“Serikali ina mipango ya ununuzi na muombaji hupata mahitaji aliyoomba ndani ya siku 14 na 45 na siyo kweli kuwa fedha zao zinang’ang’aniwa,” alisema Kusiluka.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment