MAHAKAMA
ya mkoa wa Katavi imetaifisha ng’ombe 1,312 walioingizwa na kuchunga
ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa huku washtakiwa watatu
wakinusurika kutumikia vifungo vya miaka miwili jela baada ya kulipa
faini kati ya Sh 500,000 na 700,000.
Katika
shauri la kwanza mfugaji, Shigera Mayunga (22) amenusurika kifungo cha
miaka miwili jela baada ya kulipa faini ya Sh 700,000 katika Mahakama ya
mkoa wa Katavi huku ikimwachia kwa masharti mdogo wake, mwenye umri wa
miaka 12 .
Washtakiwa
hao wawili walitiwa hatiani na mahakama hiyo kwa makosa ya kuingiza
ng’ombe 532 na kuchungia ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa.
Hakimu
Odira Amworo akitoa hukumu hiyo pia aliamuru kutaifishwa kwa ngo’mbe
wote 532 na kusema kuwa amelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho
kwa wafugaji wengine wenye tabia kama hiyo.
Awali
Mwendesha Mashtaka, wakili wa serikali Achiles Mulisa alisema
washtakiwa hao wawili walitenda makosa hayo Machi , 2016 ambapo kwa
pamoja waliingiza mifugo yao na kuchunga ndani ya hifadhi ya wanyamapori
ya Rukwa kinyume cha sheria .
Katika
shauri la pili wafugaji wawili, Ngusa Keleja “Mtungi” na Charles
Mtokambali (40) wamenusurika kutumikia kifungo cha miaka miwili jela
baada ya kila mmoja wao kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kuingiza ng’ombe
780 na kuchunga ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa .
Akitoa
hukumu hiyo , Hakimu Amworo pia aliamuru kutaifishwa kwa ng’ombe wote
780 na kuwa amelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wafugaji
wengine wenye tabia kama hiyo.
Awali
Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali , Mulisa alisema washtakiwa hao
wawili walitenda makosa hayo Machi 25, 2016 ambapo kwa pamoja waliingiza
mifugo yao na kuchunga ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa kinyume
cha Sheria.
0 comments:
Post a Comment