MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kuchunguzwa kwa sukari
kontena 115 ambayo ni zaidi ya tani 3,000 iliyokutwa katika bandari kavu
ya PMM iliyopo eneo la Vingunguti.
Makonda
alitoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika
bandari hiyo na kubaini uwepo wa sukari hiyo ambayo ni mali ya Mohamed
Enterprises, ambayo kwa taarifa zake aliambiwa zilikuwa kontena 165.
Alisema
anazitaka mamlaka zinazohusika kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Shirika
la Viwango (TBS) kuichunguza sukari hiyo kutokana na sababu mbalimbali
zilizojitokeza katika uwepo wa sukari hiyo kama sukari kuagizwa kutoka
Dubai lakini imetoka Brazil na imepakiwa Dubai, na upangwaji wa kontena
hizo katika bandari hiyo.
“Nashindwa
kuelewa kwa nini sukari iagizwe kutoka Dubai lakini itoke Brazil na
kufungashwa Dubai inaonesha inaweza kuwa imeshawahi kuisha muda wake
hivyo nataka ichunguzwe na tunataka tujue kama Mohamed Enterprises
anaficha sukari ili ipelekwe kwa wananchi kwa matumizi,” alisema Makonda.
Mbali
na kutoa maagizo hayo, Makonda pia amezuia kutumika kwa sukari mifuko
22,000 iliyokutwa katika ghala la Mohamed Enterprises Tanzania Limited
(MeTL) lililopo Barabara ya Nyerere na kutaka wapeleke vielelezo kuhusu
sukari hiyo kwa mamlaka zinazohusika kama ya matumizi yoyote.
Alisema
sukari hiyo inayodaiwa kuwa ni ya viwandani ni lazima iangaliwe kama
kweli ipo kwa ajili ya mahitaji ya viwandani au ilikuwa itumike tofauti
na ilivyokusudiwa.
Kwa
upande wake, Meneja Operesheni wa bandari kutoka MeTL, Firoz Ebrahim
alisema sukari hiyo imefuata taratibu zote na imefika katika bandari
hiyo wiki moja iliyopita.
Katika
hatua nyingine, Kampuni ya Al Naeem iliyopewa agizo la saa 36 kuanzia
juzi iwe imeshaanza kusambaza sukari kwa bei elekezi iliyokuwa katika
bandari ya Dar es Salaam, imeanza kutekeleza agizo hilo jana jioni.
0 comments:
Post a Comment