Wakati Serikali ikiendelea kuwaadhibu wafanyabiashara wakubwa kwa madai
ya kuficha sukari katika maghala, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Kutetea Walaji Tanzania (TCSA), Benard Kihiyo amesema hatua za kuwasaka
ni nzuri lakini itaharibu usambazaji na upatikanaji wa bidhaa hiyo.
Kauli
ya Kihiyo imekuja wakati msako dhidi ya wanaoficha sukari ukiwa
umepambamoto. Jana, mfanyabiashara wa Arusha, Romanus Macha alisalimisha
tani 33 za bidhaa hiyo serikalini.
Akizungumza baada ya
kutembelewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Arusha, Macha
alisema ameamua kusalimisha sukari hiyo ikiwa ni kufuata agizo la
Serikali. Alisema alitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa na wa wilaya kuwa ana
sukari.
“Mfuko wa kilo 50 nilinunua kwa Sh90,000, nilitegemea
kuuza Sh92,000. Kwa kuwa nimeshaisalimisha nasubiri bei elekezi ya
Serikali,” alisema Macha.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha,
Daniel Machunda alisema maofisa wake hawakukuta dosari kwenye sukari
hiyo lakini wanasubiri ripoti ya polisi kabla ya kuruhusu iuzwe.
“Pia tunataka kujua kama sukari hii ina ubora kwa matumizi ya binadamu,” alisema Machunda.
Katika
msako huo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na polisi
jana iliwakamata wafanyabiashara tisa waliokuwa wakiuza sukari kinyume
na bei elekezi ya Sh1,800 kwa kilo.
Tani 27 zakamatwa
Jijini Dar
es Salaam, mifuko 1,092 sawa na tani 27 za sukari ilikamatwa jana
maeneo ya Manzese baada ya msako ulioendeshwa na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya ya Kinondoni.
Msako huo ulioongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Salum Hapi ulibaini shehena hiyo katika maghala zaidi ya matatu yasiyo rasmi.
Hapi alisema, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, waliendesha operesheni hiyo na kuwabaini walioficha sukari.
“Tumeikuta kwenye viroba vya kilo 25 katika maghala mbalimbali likiwamo la Mtaa wa Mferejeni,’’ alisema.
Wataalamu
wakosoa
Wakati polisi na viongozi wengine wakihaha kuwasaka
wafanyabiashara hao, wataalamu wameeleza kuwa janga la sukari linatokana
na kukosekana kwa sera ya kumlinda mlaji.
Kihiyo alisema kama sera hiyo
ingekuwapo, wafanyabiashara wasingekuwa na nguvu ya kuuza sukari kwa
bei wanayotaka au kufanya bidhaa hiyo iwe adimu sokoni.
Hata
hivyo, maoni hayo yalitofautiana na ya mtaalamu wa masuala ya viwanda na
biashara, Adam Zuku ambaye alisema suala la sukari lina siasa ndani
yake.
Zuku ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi wa maendeleo ya
viwanda wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA),
alishangaa kuona sukari iliyokamatwa inaachiwa kwa madai kwamba,
wafanyabiashara husika hao walikuwa hawajakamilisha taratibu za kuitoa.
“Mbona
wakati tunalalamika hakuna sukari hawakusema kwamba wameagiza sukari
wanamalizia taratibu ili isambazwe madukani?” alihoji Zuku.
Alisema jambo hilo linatokana na wafanyabiashara hao kujali masilahi yao binafsi. “Wanalalamika kisiasa tu,” alisema Zuku.
Alisema Serikali isipoendelea kuvalia njuga suala hilo, hata viwanda vya sukari vya ndani vitakufa.
Pia,
alisema Serikali inatakiwa kuwa na takwimu halisi ya sukari
inayohitajika nchini ili kusiwe na mkanganyiko linapotokea tatizo kama
hilo.
0 comments:
Post a Comment