Kampuni
ya simu ya MIC Tanzania (Tigo) imekata rufaa kupinga hukumu iliyoamuru
iwalipe Sh2 bilioni wanamuziki wawili, Ambwene Yesaya na Hamisi Mwinjuma
kutokana na kutumia bila ya ridhaa yao, nyimbo za wasanii hao nyota
nchini.
Yesaya,
ambaye ni maarufu kwa jina la kisanii la AY na Mwinjuma anayejulikana
kwa jina la MwanaFA, walifungua kesi hiyo ya madai kwenye Mahakama ya
Wilaya ya Ilala kupinga kitendo cha kampuni hiyo ya huduma za simu
kutumia nyimbo zao kwenye miito ya simu bila ya ridhaa yao.
Nyimbo mbili zilizotumika kwenye miito hiyo ya simu ni “Dakika Moja” na “Usije Mjini” ambazo nyota hao wameshirikiana.
Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Juma Hassan alitoa hukumu ya kesi hiyo
Aprili 11, akiwapa ushindi wasanii hao maarufu katika muziki wa vijana
uliopachikwa jina la Bongo Fleva.
Katika
hukumu hiyo, Mahakama iliiamuru Tigo kulipa Sh5 milioni kama faini ya
uharibifu na kulipa Sh2.16 bilioni kama faini ya jumla.
Iwapo
wasanii hao watashinda rufani hiyo, watakuwa wameandika historia katika
matumizi ya Sheria ya Haki Miliki na watakuwa wasanii wa kwanza wa
muziki wa kizazi kipya kufungua kesi na kushinda.
Katika
rufaa hiyo, Tigo kupitia kampuni ya Law Associates imeainisha sababu
saba za rufani, ikidai hakimu wa Mahakama ya Ilala alikosea kisheria
kuwapa ushindi wasanii hao kwa kuwa hawakuthibitisha madai yao wala
hasara waliyopata.
Kampuni
hiyo pia inadai kuwa mbali na kutoeleza hasara waliyoipata kutokana na
kazi zao kutumika kwenye miito ya simu, walitakiwa kueleza faida ambayo
wangepata kama kazi zao zisingetumika kwenye miito hiyo.
Sababu nyingine ya Tigo kukata rufaa hiyo ni wasanii hao hawakuwa wamesajili kazi zao Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota).
Tigo
inadai kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, wadai walisema
wamesajili kazi hizo, lakini waliwasilisha barua ya Baraza la Sanaa
(Basata) ya kutambua kupokea kazi zao na si cheti cha usajili cha
Cosota.
Kwa
mujibu wa Tigo, wanamuziki hao walipaswa kuwasilisha mahakamani cheti
cha usajili wa Cosota ambako kuna utaratibu wa kujisajili ikiwa ni
pamoja na kujaza fomu maalumu baada ya kulipia malipo ya usajili ya kila
mwaka.
Kampuni
hiyo inasisitiza kuwa wasanii hao hawakuwa na haki ya kudai fidia hiyo
wakati hawajasajili kazi hizo Cosota na hivyo kuiomba Mahakama Kuu
itengue hukumu iliyowapa ushindi.
Akizungumzia hukumu iliyowapa ushindi, MwanaFA alisema huu ni wakati wa mabadiliko.
“Wale waliokuwa wanachukulia Sheria ya Hakimiliki kama mzaha, watambue kwamba zama zimebadilika,”
alisema nyota huyo wa muziki wa rap ambaye aliingia kwenye muziki
akijitambulisha kama Mwanafalsafa kabla ya kufupisha jina lake na kuwa
MwanaFA.
“Hakuna
anayetilia maanani kutumia kazi za wasanii bila ridhaa yao huku
akinufaika na wasanii kubaki wanalialia. Huu ni wakati wa kutambua kuwa
inawezekana kupata haki yako iwapo utasimama kidete kuitetea kwa sababu
sheria zipo.”
Akisisitiza,
AY ambaye pia ni nyota katika muziki wa rap aliyeimba R&B
akishirikiana na Diamond katika siku za karibuni, alisema huo ni mwanzo
wa wasanii kufunguka masikio na kutambua haki zao.
Alisema wasanii wamekuwa wakilalamika juu ya haki za kazi zao, lakini hawachukui hatua.
“Wakati ni sasa, muziki ni kazi kama kazi nyingine na ni ajira pia, hivyo unastahili kuheshimiwa,” alisema AY
0 comments:
Post a Comment