AMIRI
Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho
ya Siku ya Mashujaa Kitaifa, yatakayofanyika mjini Dodoma leo.
Hiyo
itakuwa ni mara ya kwanza kwa maadhimisho hayo kufanyika nje ya Jiji la
Dar es Salaam, tangu Tanzania ipate Uhuru wake mwaka 1961.
Pia, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuongoza maadhimisho hayo tangu alipochaguliwa Oktoba mwaka jana.
"Maadhimisho
ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma
katika Uwanja wa Mashujaa siku ya Jumatatu (leo) Julai 25, 2016 kuanzia
saa 1 kamili asubuhi hadi saa 4:30 asubuhi.
“Mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli," alisema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, jana.
Alisema
anaishukuru serikali kwa kuupatia mkoa huo, ambao ni Makao Makuu ya
nchi, heshima ya kipekee katika historia ya nchi ya kuwa mwenyeji wa
maadhimisho hayo kitaifa.
Rugimbana
alitaja shughuli zitakazofanyika siku hiyo kuwa ni gwaride la
maombolezo litakaloshirikisha vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama
vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),
Polisi na Magereza.
Kutakuwa
pia na upigaji mizinga na uwekaji wa silaha za asili na shada la maua
kwenye mnara, kama ishara ya kumbukumbu kwa mashujaa. Shughuli nyingine
ni utoaji wa dua na sala, utakaofanywa na viongozi wa madhehebu ya dini.
Rugimbana
aliwataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwenye
Viwanja vya Mashujaa kushiriki kwenye maadhimisho hayo. Alisema hadi
jana, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya shughuli hiyo yalikuwa
yamekamilika.
0 comments:
Post a Comment