Baadhi ya mabasi ya mikoani katika moja ya kituo cha mabasi nchini.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)
imesitisha leseni za madereva 18 kutokana na mgomo walioufanya kupinga
wenzao kupelekwa mahakamani.
Aidha,Wamiliki wa mabasi 12 ambayo madereva hao walikuwa wanaendesha
kwenda sehemu mbalimbali nchini, wamepewa siku saba kujieleza ni kwa
nini wasifutiwe leseni za kutolea huduma hizo pamoja na kutakiwa
kusitisha ajira kwa madereva hao.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed
Mpinga, alisema Julai 23 mwaka huu mkoani Kagera, madereva wa mabasi
hayo walifanya mgomo kupinga kitendo cha madereva wenzao kupelekwa
mahakamani, kukosa dhamana na kulala rumande kutokana na makosa
mbalimbali ya usalama barabarani ikiwamo kuendesha kwa mwendo kasi.
Kamanda Mpinga alisema dereva yeyote atakayeendesha gari kwa kasi ya
zaidi ya kilometa 90 kwa saa atafikishwa mahakamani na sio kutozwa faini
kama awali ili kuhakikisha matukio ya ajali yanapungua nchini.
Alisema kutokana na hali hiyo madereva wanaoendesha mabasi yanayoanza
safari zake kwenye Manispaa ya Bukoba, walisitisha huduma kwa
kushinikiza Mahakama iwaachie wenzao waliokamatwa kwa makosa ya mwendo
kasi.
Naye Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard Ngewe, aliyataja mabasi pamoja
na madereva waliositishiwa leseni kuwa ni Hussein Tegatega na Miraji
Kondo wa Kampuni ya RS Express wanaoendesha basi lenye namba za usajili T
425 DDT aina ya Zongtong linalotoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Said Omary na Amos Danney wa basi la Kimotico lenye namba za usajili T
966 CDY aina ya Nissan linalotoka Bukoba kwenda Arusha na madereva
wanne wa mabasi ya Princess Muro yenye namba za usajili T 166 DCA na T
923 DCT yanayosafiri kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Madereva hao ni Ally Mshuza, Twalibu Ondossy, Costa Andrew na Witness Lema.
Wengine ni Musa Tindwa na Gerald Beti wa Kampuni ya Osaka Raha
wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 968 CPC linalofanya safari
zake Bukoba kwenda Dar es Salaam na Paul Ngussa wa basi lenye namba za
usajili T 810 BDW aina ya Scania linalotoka Bukoba kwenda Musoma, mali
ya Kampuni ya Bunda Express.
News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia
Facebook
,
Twitter na
Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.
0 comments:
Post a Comment