NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Vitu alivyoongea bilionea Mohammed Dewji katika mpango wake wa kuinunua Timu Ya Simba


Kuelekea mkutano mkuu wa Simba unaotaraji kufanyika Jumapili ya Julai, 31, shabiki na mkeleketwa wa Simba ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji amezungumza mipango yake aliyopanga kuifanyia Simba kama akipata nafasi ya kununua hisa asilimia 51 za klabu hiyo.

MO amesema kuwa mipango yake ni kuwekeza Bilioni 20 na amepanga bajeti ya klabu hiyo kwa mwaka iwe Bilioni 5.5, kiasi ambacho anaamini kuwa kitaweza kubadili mwelekeo wa Simba kutoka ilivyo sasa na kurudisha zama zake za kutwaa mataji ya ndani na kufika hatua nzuri kimataifa.

MO alisema amefikia uamuzi wa kutaka kununua hisa katika klabu ya Simba kutokana na mapenzi aliyonayo katika klabu hiyo na hana nia yoyote ya kiabiashara na klabu hiyo kwani tayari ana biashara anazofanya ambazo zinamuingizia pesa nyingi hivyo jambo hilo ni kuona timu aliyo na mapenzi nayo ikifanikiwa.

“Nipo tayari kuwekeza Bilioni 20 kama watanipa nafasi lakini tukubaliane kuwa hakuna mtu atagusa pesa hizo pesa, tutauza bondi na kwa kila mwaka tutaingiza Bilioni 3.5 na tutatengeneza mapato ya Bilioni 2 kila mwaka ukijumlisha ni Bilioni 5.5 ambayo itakuwa ni bajeti ya mwaka,

“Inaniuma sana kuona klabu imekuja juzi tu leo inatuzidi mafanikio lakini kama Yanga na Azam bajeti zao kwa mwaka ni Bilioni 2.5 hadi Bilioni 3, sisi tukiwa na bajeti ya Bilioni 5.5 tutakuwa tumewazidi na tutaleta wachezaji wazuri na kocha mzuri,” alisema na kuongeza.

“Dhamira yangu sio kupata Simba kibiashara, mimi Mungu kanijalia nina pesa nina biashara ziadi ya 100, tumeajiri wafanyakazi wanafika 28,000 , jambo ninalolitaka Simba ni kuwekeza, tubadili mfumo, tushinde mataji na sio Tanzania pekee shabaha yangu ni kushinda mataji ya Afrika”

Aidha MO alisema kuwa kama akipata nafasi atazungumza na viongozi wa Simba ili kila mwanachama wa klabu wa muda mrefu apatiwe hisa bure kutokana na kazi kubwa ambayo wameifanya katika klabu hiyo.

“Nitazungumza na viongozi wa klabu tuone jinsi ambavyo tunaweza kuwapa bure wanachama wa klabu ambao wamekuwa na timu kwa muda mrefu, wameshatoka jasho sana na Simba hivyo tutawapa hisa za timu bure,” alisema MO.

Hata hivyo MO aliongeza kuwa yupo tayari kwa lolote kama katika mkutano mkuu wa Jumapili watamnyima nafasi ya kuwekeza katika klabu ya Simba na kueleza kuwa anachoamini kwa sasa Simba haiitaji mdhamini bali Simba inahitaji mwekezaji.

“Mimi wakininyima kwa moyo mweupe kabisa sina tatizo na hili jambo hata likifanikiwa halitakamilika kesho linaweza kuchukua muda sababu kuna mambo ya kufanyiwa marekebisho na kusaini mikataba ila kama nikiona mambo yanakwenda sawa kwa hicho kipindi nitaangalia jinsi gani nitaisaidia Simba sababu nina mapenzi nayo,” aliongeza MO.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment