MMOJA
wa madereva waliosababisha ajali ya mabasi ya Kampuni ya City Boy
iliyotokea Julai 4, mwaka huu na kutoroka, Boniface Mwakalukwa (37),
amejisalimisha mikononi mwa polisi na kufikishwa mahakamani.
Mwakalukwa
ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam jana aliunganishwa kwenye
mashitaka na dereva mwenzake Jeremiah Semfungwe (34) wote kwa pamoja
wakikabiliwa na makosa 30 ya kuua bila kukusudia.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida,
Joyce Minde ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo Julai
4, mwaka huu saa 8.15 mchana wakati wakiendesha mabasi aina ya Scania
yenye namba za usajili T 247 BCD na T 331 DCE kwa kuyagonganisha.
Ilidaiwa
kuwa kitendo hicho ambacho kilitokea Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni
kilisababisha vifo vya abiria 30 na majeruhi 54. Wakili wa Serikali,
Petrida Muta alidai kuwa siku ya tukio watuhumiwa wakiwa ni madereva wa
Kampuni ya City Boys, bila kukusudia, walisababisha vifo vya abiria hao
kinyume na Kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Toleo la
Kwanza.
Ingawa
Wakili wa washitakiwa, Francis Kitope aliiomba Mahakama iwape wateja
wake dhamana kwa kuwa chini ya Kifungu 148 cha Mwenendo wa Makosa ya
Jinai, kosa hilo linadhaminika, Wakili wa Serikali Muta alipinga dhamana
hiyo.
Muta
ambaye aliwasilisha Hati ya Kiapo mbele ya Mahakama hiyo, alidai kuwa
kwa kufanya hivyo usalama wa washitakiwa utakuwa hatarini kwa kuwa ndugu
wa marehemu na majeruhi bado wana hasira kutokana na ajali hiyo kuwa
bado haijasahaulika.
Aidha,
Muta aliendelea kudai kuwa baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo hali zao
bado ni mbaya na hatma yao haijulikani, hivyo si vyema washitakiwa
kupewa dhamana wakati huu. Kutokana na upelelezi wa kesi hiyo
kutokamilika, washitakiwa wamerejeshwa rumande hadi Agosti 4, mwaka huu
kesi yao itakapotajwa tena.
0 comments:
Post a Comment