Katibu
Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome amesema kuanzia
sasa sheria zote zitakazotungwa nchini zitakuwa katika lugha ya
Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi ambao ndio walengwa wa sheria
hizo, kuzielewa.
Uamuzi
huo unakwenda sambamba na kuzitafsiri sheria zote zinazotumika nchini
ambazo ziko katika lugha ya Kiingereza ili kutimiza lengo hilo la
kuwafanya wananchi wengi wazielewe.
“Kwa
sasa serikali imeamua kuwa sheria zote nchini zitakuwa katika lugha ya
Kiswahili na zile ambazo ziko katika lugha ya Kiingereza zitatafsiriwa
ili kuwawezesha Watanzania wengi ambao ndio walengwa wa sheria hizo
kuzielewa,” alisema.
Pia
alisema serikali itazifanyia marekebisho sheria zote ambazo zimekuwa
zikilalamikiwa na wadau mbalimbali kuwa hazikidhi mahitaji au haja,
haziendani na wakati uliopo sasa ili kutekeleza azma yake ya kuwahudumia
wananchi wake kwa ukamilifu.
Profesa
Mchome ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana baada ya kupokea
mapendekezo yaliyowasilishwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na
Maendeleo Afrika (WILDAF), ambayo yanataka kufutwa kwa sheria mbalimbali
za kimila zinazosimamia masuala ya mirathi ambazo zinalalamikiwa
kuwakandamiza wanawake nchini.
Profesa
Mchome amewashukuru WILDAF kwa kazi waliyoifanya na kuwaahidi kuwa
wataalamu wake wizarani watayafanyia kazi mapendekezo yao ili
kuhakikisha gurudumu la sheria nchini linasonga mbele na kuwasaidia
wananchi wengi.
Akizungumza
katika makabidhiano hayo Mkurugenzi wa WILDAF, Judith Odunga alisema
mapendekezo hayo yanataka kufutwa kwa sheria za kimila ambazo kwa kiasi
kikubwa zimekuwa zikiwakandamiza wanawake, kuwanyima haki ya kumiliki
mali na kufanyiwa vitendo vya kidhalilishaji pale wanapofiwa na waume
zao.
Alisema
katika mapendekezo hayo WILDAF inaiomba serikali itunge sheria moja
ambayo pamoja na zile za kidini itashughulikia masuala ya mirathi na
kuweka usawa wa kisheria katika urithi wa mali kati ya mwanamke na
mwanamume, ikiwa ni pamoja na watoto wa kiume na wa kike kuwa na usawa
katika kurithi mali inapotokea mzazi wa kiume amefariki dunia.
0 comments:
Post a Comment