Tetemeko
la ukubwa wa mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7 limetokea katika mikoa
mitatu nchini na watu zaidi ya 10 wamekufa na wengine 120 wamejeruhiwa
huku majengo mengi yakibomoka.
Mikoa
iliyoripotiwa kuathiriwa kwa tetemeko hilo ni Kagera, Mwanza na Mara.
Pia tetemeko hilo limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda jana
saa 9.27 alasiri.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema tetemeko hilo
limetokea saa tisa alasiri na zaidi ya watu 10 wamekufa.
Awali,
akizungumza kwa simu kutoka jiijini Dar es Salaam, Kamanda Ollomi
alisema watu wanane walikufa na baadaye alisema idadi hiyo iliongezeka
na kwamba alipata taarifa kutoka hospitali ya mkoa kuwa wamepokea miili
ya watu 10 na wameihifadhi.
Alisema tisa kati ya waliokufa ni wakazi wa Manispaa ya Bukoba na mmoja ni mkazi wa wilayani Karagwe.
Kamanda
alisema miongoni mwa majeruhi wamo wanafunzi 15 wa Shule ya Sekondari
ya Wavulana Ihungo na wapo katika hospitali ya mkoa wanaendelea kupatiwa
huduma. Alisema bado vikosi vya uokoaji likiwemo Jeshi la Polisi na
Zimamoto vinaendelea na uokoaji.
Alisema watu waliojeruhiwa na waliokufa wamedondokewa na kuta, vifusi na vyombo vya ndani.
Alisema wengine walikufa kwa mshituko unaosababishwa na shinikizo la damu na nyumba zaidi ya 40 zimeathirika.
“Ni
kweli tetemeko la ardhi limetokea na kusababisha uharibifu mkubwa wa
mali za watu, vifo pamoja na majeruhi na bado tunaendelea kupokea
taarifa zaidi,” alisema Kamanda Ollomi na kuongeza kuwa mpaka jana
jioni walikuwa wakiendelea kupokea taarifa kutoka sehemu mbalimbali za
mkoa huo kuhusu vifo na majeruhi.
Wakala wa Jiolojia waelezea ukubwa wake
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma
alisema tetemeko hilo ni kubwa kwa nusu ya kipimo cha juu cha Ritcher10
na limezidi kipimo cha chini cha ukubwa wa Ritcher tatu. Alisema
limezidi lililotokea Dodoma hivi karibuni.
Profesa
Mruma alisema tetemeko hilo limetokea katika mpaka wa Tanzania na
Uganda, kilometa 47 kaskazini mwa Bukoba mkoani Kagera na sababu ni
mpasuko wa ardhi katika Bonde la Ufa la magharibi karibu kabisa na Ziwa
Victoria .
Amewataka
wananchi kuchukua tahadhari kwani kwa kawaida linapotokea tetemeko
kubwa kama hilo hufuatiwa na matetemeko madogo na ardhi hutulia baada ya
siku mbili mpaka tatu.
“Kwa
wakati huu ili kuepuka madhara zaidi, litakapotokea watoke nje ya
nyumba na kukaa mbali na miti kwenye uwanja wa wazi na wanaoendesha
magari waache mara moja,” alisema Profesa Mruma.
Alisema
kwa sasa wataalamu katika kituo chao cha kupimia matetemeko cha Geita
wanaendelea kupata takwimu zaidi kutokana na kuwa mpasuko wa tetemeko
hilo umekuwa karibu sana na ziwa Victoria na baadaye watatoa taarifa
kuhusu tukio hilo kwa undani.
0 comments:
Post a Comment