Wanafunzi wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari Usevya wilayani Mlele
Mkoa wa Katavi, wanadaiwa kuwashambulia kwa kuwacharaza viboko walimu
wao wawili miongoni mwao akiwemo Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Makonda
Ng’oka “Membele’‘ (34) ambaye ameng’olewa meno matano kwa kipigo hicho.
Walimu hao wawili wamedai kuwa hawako tayari kuendelea kufundisha
katika shule hiyo huku wakisisitiza kuwa ni fedheha kwao kucharazwa
viboko na wanafunzi wao wenyewe ambapo Mwalimu Gabriel Kambona aliachwa
na ngeu kichwani.
Mei mwaka huu, Ng’oka “Membele” alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa
wa Katavi kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake akidaiwa kutenda kosa
hilo kati ya Novemba 2015 na Aprili mwaka huu.
Ilisemekana kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Makamu Mkuu huyo
wa shule hiyo kulifuatia wanafunzi wa kiume wanaosoma Kidato cha Tano
sasa wako Kidato cha Sita katika shule hiyo kumkataa na kutishia
kuandamana kupinga vitendo vyake vya kuwalawiti wanafunzi wake.
Wanafunzi hao walidai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwalawiti baadhi
yao ikiwa ni adhabu mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni hapo.
Hata hivyo, baada ya kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani Ng’oka,
Julai 27, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda
ilimwachia huru.
Mwalimu Ng’oka aliripoti kwenye kituo chake cha kazi shuleni Usevya
Agosti Mosi mwaka huu ambako kurejea kwake shuleni hapo kunadaiwa
kuamsha hasira kwa baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wakidai hawapo
tayari kumwona mwalimu huyo na familia yake shuleni hapo.
Mwalimu Ng’oka aliliambia gazeti la Habari Leo kuwa hayuko tayari
kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo akihofia usalama wake na kutokana
na kipigo alichokipata cha kushambuliwa na baadhi ya wanafunzi wake wa
kidato cha tano na cha sita wakati akiwa nyumbani kwake na familia yake.
Akisimulia mkasa huo, alisema Agosti 12, mwaka huu usiku alikuwa
nyumbani kwake shuleni hapo pamoja na familia yake pamoja na mwalimu
mwenzake, Gabriel Kambona aliyekuwa amemtembelea.
“Ghafla, saa mbili usiku nikiwa maliwatoni nikioga lilitokea kundi la
wanafunzi wa kidato cha tano na sita wakiwa na silaha za jadi kama vile
fimbo, marungu, mawe na matofali na kuanza kuishambulia familia yangu
pamoja na mwalimu Kambona,” alieleza na kuongeza kuwa alilazimika
‘kuchomoka’ bafuni baada ya kusikia mayowe yaliyokuwa yakipigwa na
familia yake wakiomba msaada. Alipofika sebuleni alishuhudia wanafunzi
hao wakiishambulia familia yake kwa kuwacharaza viboko.
“Ndipo walinigeukia na kuanza kunishambulia kwa kunipiga kwa marungu
na fimbo hadi nikapoteza fahamu nilizinduka nikiwa nimelazwa kwenye
Kituo cha Afya Usevya na kubaini kuwa nimepoteza meno yangu matano huku
nikiwa nimejeruhiwa vibaya kichwani. Baadaye nilihamishiwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako nililazwa wiki moja na nusu kwa
matibabu na sasa nimepewa rufaa niende Hospitali ya Taifa Muhimbili
jijini Dar kwa matibabu zaidi,” alieleza.
Alidai kuwa uhasama baina yake na wanafunzi hao umedumu kwa muda
mrefu, lakini anashangaa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya
Mlele umeshindwa kumpangia kituo kingine cha kazi na kuchukua hatua
yoyote kwa wanafunzi hao licha ya kupeleka majina yao kwa kuwa
anawafahamu wote waliohusika.
Mwalimu Kambona alidai kuwa hayuko tayari kuendelea kufundisha kwenye
shule hiyo kwamba kitendo cha kupigwa na wanafunzi wake
kimemfedhehesha.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, walimu wa shule hiyo waliketi baada ya
kutokea kwa tukio hilo, na walifikia maamuzi kuwa wanafunzi wote
waliobainika kushiriki kuwashambulia walimu wao wasimamishwe shule
akidai kuwa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele
ulipinga.
“Nimeandika barua ya kuomba uhamisho kwani nia aibu kwangu kuendelea
kufundisha wanafunzi ambao wamenishambulia na kunitoa ngeo kichwani …..
siku hiyo ya tukio niliibiwa simu mbili za kiganjani lakini jana
nimefanikiwa kuikamata simu moja kwa mwanafunzi wa kidato cha tano
anayeitwa , Alex Maiko Makona na tayari amemfikisha katika Kituo cha
Polisi cha Usevya,” alidai.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Katavi, Gregori Mshota
alisema tayari chama
chake kimeanza kuwasiliana na uongozi wa
Halmashauri ya Mpimbwe na uongozi wa Wilaya ya Mlele ili kuhakikisha
mwalimu huyo anakuwa salama.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa nje ya mkoa, Ofisa
Elimu wa Mkoa wa Katavi, Ernest Hinju alidai kuwa suala hilo lipo
ofisini kwake na wameanza kulitafutia ufumbuzi. “Jambo hili linahitaji
ushirikishwaji wa vyombo mbalimbali ikiwemo Bodi ya Shule ya Sekondari
ya Usevya,” alieleza
Source: Habari Leo
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment