NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Tanzania yaanza kuandaa kikosi kipya cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17

Tanzania imeanza kuandaa kikosi kipya cha timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys kitakachoshindana kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka hiyo.
caf
Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), limeiteua Tanzania kuandaa fainali hizo mwaka 2019 hivyo sasa TFF imeanza kuandaa vijana wake.

Kwa kuanzia tu, imeanza kuwamulika vijana 22 wanaosoma Shule za Alliance zilizoko Mwanza.
Mapema wiki hii, ilimuagiza Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu kwa Vijana, Kim Poulsen kupima uwezo wa vijana hao kwa kufanya nao mazoezi kwenye viwanja vya Alliance ambako alimaliza na kusema: “Tuna timu bora ya taifa.”

“2019 si tu kwamba Tanzania itashiriki, bali kushindana. Lakini naipongeza TFF na Alliance kwa kuanza program ya kuandaa timu bora. Serengeti Boys ya sasa inayomaliza muda wake iliandaliwa kwa mwaka mmoja, lakini vijana hawa wenye umri wa miaka 12 na 13 ni hazina nyingine kubwa kwa taifa…

“Kwa jinsi nilivyowaona itoshe kusema tu tayari tuna timu. Nimesikia viongozi wa TFF wakisema kwamba jicho lao si kwa vijana hawa tu, bali pia kwa vijana wengine Tanzania nzima.

Hili ni jambo zuri lenye manufaa mazuri,” amesema Poulsen alipozungumza na waandishi wa habari leo mara baada ya mazoezi ya asubuhi.

Nahodha wa timu hiyo ya vijana, alishukuru Alliance kwa malezi mazuri na TFF kwa kuendelea kuwajali hasa kwa sasa ambako nao wamesema ndoto zao ni kutaka kung’ara zaidi ya Serengeti ya sasa ambao walitolewa na Congo Brazzaville katika harakati za kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika, zitakazofanyika mwakani nchini Madagascar.

Vijana waliotolewa kwa sasa wanajipanga upya kwenda Korea Kusini kwa ajili ya kujiandaa na ratiba mpya ya CAF na FIFA kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 ambako timu ya taifa kwa hapa Tanzania inaitwa Ngorongoro Heroes. Ratiba za michuano ijayo ya kimataifa, itatolewa baadaye mwaka huu.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment