Mwenyekiti mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda ametamba kuwa ataimarisha uhusiano wa kisiasa kati ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.
Shibuda ambaye ni Katibu
Mkuu wa Chama cha Ada Tadea, alitoa tambo hizo jana, ikiwa ni dakika
chache baada ya kuchaguliwa kuongoza baraza hilo kwa kipindi cha miaka
miwili katika uchaguzi uliofanyika jijini Dar akichukua nafasi ya Peter
Kuga Mziray wa APPTMaendeleo kilichofutwa na Msajili wa Vyama vya
Siasa.
Shibuda alisema atatumia fursa, uzoefu na uwezo alionao
kuhakikisha vyama vyote vinakuwa na matumaini ya ushiriki wa kisiasa
kupitia heshima ya baraza hilo.
“Nimepokea kwa furaha matokeo haya
lakini najua nina mzigo mbele yangu. Hilo la mahusiano ninamtanguliza
Mungu anisaidie ili kuhakikisha naotesha matumaini mapya katika baraza
hili. Nitakunjua vizibo vyote vilivyoziba katika mahusiano haya,
ushirikiano wa siasa zetu uwe kwa masilahi ya Watanzania na utaifa
wetu,” alisema mbunge huyo wa zamani wa CCM na Chadema.
Shibuda aliibuka
mshindi baada ya kupata kura 20 dhidi ya mpinzani wake, Mwenyekiti wa
CCK, Constantine Akitanda aliyefuata kwa kura 14.
Jumla ya kura 36
zilipigwa huku mbili zikiharibika. Katibu wa CCK, Renatus Muabhi
alipongeza ushindi wa Shibuda huku akitoa angalizo kuwa asikubali
kutumika kulinda masilahi ya kundi la chama kilichopo madarakani.
“Namwamini kwa uzoefu wake atasaidia kurejesha heshima ya baraza hilo
ila kama atayumbishwa, sisi tuko tayari kushawishi kura ya kumwondoa
madarakani,” alisema.
Wengine waliogombea kiti hicho ni Hashim Rungwe
(Chaumma), Anna Mghwira (ACT), Fahmy Dovutwa (UPDP), Hassan Kisavya
(NRA), na John Cheyo wa UDP ambaye alijitoa.
Baadhi ya vyama
vilivyoshiriki katika uchaguzi huo ni Sauti ya Umma (Sau), CUF, CCM,
DP, Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, Ada-Tadea, CCK na Chadema.
Baraza
la Vyama vya Siasa ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama
vya Siasa kwa lengo la kuweka jukwaa la kujadiliana masuala yenye
masilahi kwa Taifa na uimarishaji wa mfumo wa vyama vingi nchini.
0 comments:
Post a Comment