Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga kufuatia vifo vya watu 12
vilivyosababishwa na kuzama kwa boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Tanga
kwenda Pemba.
Ajali
hiyo imetokea usiku wa kuamkia tarehe 10 Januari, 2017 katika kisiwa
cha Jambe kilichopo katika bahari ya Hindi umbali mfupi kutoka Tanga
Mjini, ambapo pamoja na vifo vya watu hao watu wengine 33 wamenusurika
na 25 kati yao wamelazwa katika Hospitali ya Bombo Mkoani Tanga.
"Nimeshtushwa
na kusikitishwa sana na vifo vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha
katika ajali hii ya kuzama boti, tumepoteza wapendwa wetu, watoto wetu
na watu wazima ambao kwa hakika familia zao ziliwategemea katika maisha
ya kila siku, nakuomba Ndg. Mkuu wa Mkoa unifikishie pole nyingi kwa
familia za Marehemu wote na jamaa zao" amesema Dkt. Magufuli katika salamu hizo.
Aidha,
Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi
na pia amewataka wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu
na subira katika kipindi hiki cha huzuni ya kuondokewa na jamaa zao.
Dkt.
Magufuli pia amewatakia matibabu mema majeruhi wote walionusurika
katika ajali hiyo ili wapone haraka, warejee katika familia zao na
waendelee na ujenzi wa Taifa.
"Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, Amen" Amemalizia Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment