newspointtz.blog
JANA
ilikuwa siku ambayo Rais John Magufuli alitoa uamuzi mzito wa
kubadilisha nafasi za uongozi wa ngazi ya juu zaidi kwa viongozi ambao
amefanya nao kazi baada ya kumuondoa Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa
katibu Mkuu Kiongozi, akiwa mstari wa mbele kutangaza wanaotumbuliwa
majipu.
Balozi Ombeni Sefue alikuwa kivutio cha wengi kwenye vyombo vyahabari
kutokana na kutoa taarifa za kutenguliwa uteuzi kwa watumishi
waandamizi wa umma, lakini jana hali ilikuwa tofauti baada ya kibao
kugeuka.
Ombeni Sefue aliibukia
kuwa kipenzi cha vyombo vya habari katika muda mfupi aliofanya kazi na
Rais Magufuli, huku mitaani akivuta wengi karibu na runinga kila
alipoonekana, hasa kutokana na wananchi kutarajia kusikia habari za
kutumbuliwa kwa majipu ambao umekuwa ukifanywa na Serikali tangu Rais
aapishwe Novemba 5, 2015.
Alianza
kuchukuliwa na wengi kuwa ni mchapakazi na muadilifu na angeweza kwenda
na kasi ya Rais Magufuli, ambaye amekuwa akihimiza mambo hayo na
kusisitiza kuwa mtu asiyeweza kwenda na kasi yake, hatamvumilia.
Hakuna aliyekuwa na shaka na Balozi Sefue. Hata gazeti la Dira
lilipotoa habari mfululizo kwenye matoleo mawili likimuhusisha na
ushauri mbaya kwa Rais na pia utafutaji wa mjenzi wa daraja la
Kigamboni, wengi hawakuweza kuamini, hasa kutokana na kuonekana kuwa
karibu na Rais.
Lakini
uamuzi wa Rais kumteua Balozi Kijazi kushika nafasi yake, unaweza
kuibua mjadala mpya kuhusu ujenzi wa daraja hilo na mabadiliko
yanayofanywa na Rais.
Uteuzi
wa Katibu Mkuu Kiongozi mpya umekuja siku 67 tangu Rais Magufuli
atangaze kuteua makatibu wakuu 29 wapya Desemba 30, 2015 huku Sefue
akihakikishiwa kuendelea kukaa Ikulu kwa mwaka mmoja zaidi.
Uteuzi huo pia umekuja siku chache baada ya gazeti la Dira kuanza
kuandika jinsi Ikulu ilivyoshauriwa vibaya kuhusu uteuzi wa mkurugenzi
mkuu wa Bohari ya Madawa (MSD), ingawa Idara ya Habari (Maelezo) ilitoa
tamko kali la kukanusha na kulitaka gazeti hilo liombe radhi, kitu
ambacho hakijafanyika.
Uteuzi
huo pia umekuja wakati kukiwa na sarakasi ya uteuzi wa Carina Wangwe
kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa NSSF na uamuzi huo kutenguliwa saa tano
baadaye (kutangazwa saa 11:150 jioni na kutenguliwa saa 4:15 usiku).
Katika
sakata hilo, Sefue hakutangaza uteuzi huo ila alisema kuwa mamlaka ya
kuteua ni ya Rais lakini ya kukaimu kuna taratibu zake, ambazo
hakuzitaja. Alisema Wangwe alitakiwa kuwa mwangalizi.
Pia
Balozi Kijazi, ambaye anamrithi Sefue kwenye nafasi ya Katibu Mkuu
Kiongozi, ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu wakati
pendekezo la ujenzi wa daraja la Kigamboni lilipotolewa na baadaye
kupitishwa huku likikumbana na upinzani mkali toka kwa Kijazi na Magufuli ambaye wakati huo alikuwa ni Waziri wa JK.
Balozi Kijazi aliondolewa wizara hiyo na kupelekwa ubalozini nchini India mwaka 2007 huku Magufuli akihamishiwa Wizara ya Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo mwaka 2008.
Balozi
Sefue alizaliwa Agosti 26, 1954 wilayani Same, Kilimanjaro. Alisomea
Utawala na Sera za Umma kwenye Chuo cha Uongozi cha Mzumbe, ambacho sasa
kinaitwa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Baadaye
alipata shahada ya uzamili katika fani hiyo kwenye Chuo Kikuu cha
Masomo ya Kijamii cha The Hague nchini Uholanzi mwaka 1981.
Pia ana astashahada ya uzamili ya masuala ya uhusiano wa kimataifa aliyoipata Chuo cha Diplomasia kilichopo Dar es Salaam.
Pia
ana cheti cha usuluhishi wa kimataifa, matatizo ya kiuchumi na kijamii
ya nchi zinazoendelea. Balozi Sefue na mkewe Anita wana watoto wawili,
wa kiume na kike.
Amekuwa balozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2007. Kabla ya hapo, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Canada (2005-07).
Balozi
Sefue aliachana na kazi ya udiplomasia mwaka 1993 na kwenda kufanya
kazi ya kuandika hotuba za rais na pia kuwa msaidizi binafsi wa Rais Ali
Hassan Mwinyi. Baada ya uchaguzi wa mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa
aliendelea naye hadi mwaka 2005 wakati alipoachia ngazi.
Balozi
Sefue alifanya kazi kwa karibu na Mkapa wakati akiwa Kamisheni ya
Afrika (maarufu kama kamisheni ya Blair) ambayo ilitengeneza ripoti
iliyojulikana kwa jina la “Our Common Interest: Report of the Commission
for Africa in March 2005”, na kushiriki naye kwenye kikao cha marais wa
nchi nane tajiri duniani (G8) ambacho kilijadili ripoti hiyo.
Pia
alifanya kazi kwa karibu na Mkapa wakati akiwa mwenyekiti mwenza wa
kamati iliyochambua athari za utandawazi kijamii ya Shirika la Kazi
Duniani (ILO) kati ya mwaka 2002-2004.
Rais
Kikwete alimteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Desemba 31, 2011 na amedumu
na wadhifa huo mpaka jana, huku akifanya kazi na Rais wa Awamu ya Tano,
Dk Magufuli kwa siku 67 tu licha ya kuwa aliongezewa mwaka moja.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment