newspointtz.blog
Wafanyabiashara
wa sukari nchini wameanza kujenga utaratibu wa kuficha sukari ili
kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi lengo likiwa ni kushinikiza
vibabali vya kuingiza sukari kutoka nje vinatolewa.
Hatua hiyo
imemwibua Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye anakiri
kuwepo kwa hujuma hizo na kudai, serikali haitalala.
Amesema,
kuna wafanyabiashara wanaficha sukari kwenye maghala yao ili kuchochea
mfumko wa bei na kisha waiuze kwa bei ya juu na hatimaye kupata faida
kubwa.
Hivi karibuni Rais Magufuli alizuia kutolewa vibali holela
vya uingizaji sukari nchini na kumwagiza Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu
kusimamia hilo.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kwamba,
wafanyabiashara waliokuwa wananufaika na uingizaji wa sukari nchini
wameanza kuhujumu kwa kushirikiana na wenye maghala ya sukari.
Mwijage
amesema, wafanyabiashara hao wamekuwa wakificha sukari ghalani ikiwa
pamoja na kufungia maghala yao ili kuzuia mfumuko wa bei na hatimaye
kupata faida kubwa.
Amesema hayo katika mkutano na waandishi wa
habari jana jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wananchi kutoa taarifa
sahihi za baadhi ya watu wanaoendelea kuficha sukari kwa makusudi.
“Kama
kuna taarifa sahihi za baadhi ya watu wanaoficha sukari ghalani kwa
makusudi ili kuiaminisha jamii kuwa sukari ya ndani haikidhi na
kupandisha bei holela ya sukari kwa masilahi yao binafsi muwataje,”
alisema Mwijage.
Mwijage alisema kuwa, kwa dhamana aliyokuwa nayo
katika Sekta ya Viwanda na Biashara anauwezo wa kufungia maghala
yatakayobainika kuficha sukari kwa makusudi.
“Niwahakikishieni
kuwa hakuna mfumuko wa bei ya sukari, mambo ni mazuri na utaratibu uko
vizuri, niwasihi wawekezaji wa ndani wajitokeze kuwekeza katika viwanda
vya sukari ili kuiendeleza nchi yetu,” alisema.
Alisema, Serikali
inampango wa kujenga viwanda vya sukari vidogo na vikubwa ikiwemo
ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari kinachotarajiwa kujengwa hivi
karibuni katika mkoa wa Kigoma.
“Viwanda vya sukari vinakuja,nchi
yetu si ya kupokea bidhaa hafifu, sukari isiyokidhi ubora haitaingia
nchini wala kuuzwa na kutumiwa na watanzania,” alisema Mwijage.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment