NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

MAUWASA Mbaroni Kwa Ufisadi ya Milioni 108


MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Maswa (MAUWASA) mkoa wa Simiyu, Lema Jeremiah (50) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa akikabiliwa na makosa ya wizi wa Sh milioni 108 mali ya serikali.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Nassib Swedy alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Tumaini Marwa kuwa mshitakiwa anatuhumiwa kufanya wizi wa fedha akiwa mtumishi wa Umma.

Swedy alidai Machi 7 mwaka 2014 saa 3:00 asubuhi, Jeremiah akiwa katika Ofisi za Mamlaka hiyo zilizoko katika kijiji cha Sola wilayani humo aliiba Sh milioni 108 zikiwa ni mali ya Serikali zilizotolewa na Mwajiri wake ambaye ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Alisema kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 270 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Hata hivyo, mara baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa huyo alipoulizwa na hakimu Marwa kuhusika nalo, alikana kosa hilo na mwendesha mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ili waendelee na upelelezi na kesi hiyo itatajwa tena Aprili 11 mwaka huu.

Hakimu Marwa alisema masharti ya dhamana kwa mshitakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 50 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 50 na hati hiyo itatakiwa ikaguliwe kama kweli inafikia kiasi hicho.

Mshitakiwa amekidhi vigezo hivyo na kuachiwa kwa dhamana, lakini alipotoka mahakamani akashikiliwa na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa madai kuwa anahitajika  kwa mahojiano zaidi kutokana na tuhuma nyingine zinazomkabili.
 
 
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment