Mkuu
wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Amani Mwenegoha ameingilia kati kwa
kuwasuluhisha maofisa wa Takukuru na polisi waliokunjana mashati
wakimgombea shahidi katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi wilayani
hapa.
“Nimelazimika kuita kikao cha dharura cha kamati ya ulinzi na
usalama kujadili suala hili linalotishia kuvuruga uhusiano mwema kati ya
taasisi hizi mbili zinazopaswa kushirikiana,” alisema Mwenegoha.
Alisema kabla ya tukio hilo, Machi 8 mwaka huu, ofisi yake ilipokea
malalamiko kutoka Takukuru kuwa baadhi ya maofisa wa polisi walivuruga
upelelezi na ushahidi wa kesi ya tuhuma za rushwa inayomkabili mmoja wa
walimu wa shule za msingi.
“Baada ya kikao cha zaidi ya saa nne kuanzia
saa 11 jioni hadi saa mbili usiku, pande zote zimezika tofauti na
nimewapa onyo mkuu wa polisi wa wilaya na mwenzake wa Takukuru
nikiwataka kuwasimamia vyema
maofisa waliopo chini yao kuepusha tukio kama lile,” alisema mkuu huyo
wa wilaya.
Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho ni
polisi na Takukuru kuheshimiana na kushirikiana kutekeleza majukumu yao.
“Nimeagiza OCD na mkuu wa PCCB waitishe vikao vya haraka vya ndani
kujadili suala hili na kuwekana sawa,” alisema.
Mwenegoha alisema
amewapa wakuu wa taasisi hizo muda wa siku tano kuanzia Jumanne
iliyopita kukamilisha vikao vyao vya ndani na kutoa mrejesho kwenye
kikao cha kamati ya ulinzi na usalama jinsi walivyoshughulikia suala
hilo lililoitia aibu Serikali baada ya watumishi wake kukunjana mashati
hadharani.
Alisema kitendo cha askari polisi kumkamata na kumfunga
pingu shahidi wa Takukuru, Paulo Stephano kabla ya kutoa ushahidi
hakikuwa cha kiungwana wala kuheshimu mamlaka nyingine ya Serikali na
kimetoa taswira kuwa jeshi hilo lililenga kudhoofisha ushahidi wa taasisi
hiyo.
“Haikubaliki polisi kumvamia shahidi wa Takukuru, kumweka chini ya
ulinzi, kumfunga pingu na kumtupia kwenye gari lao hata kabla hajatoa
ushahidi,” alifafanua.
Kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya
wilaya hiyo kitakachopokea taarifa ya vikao vya ndani vya Takukuru na
polisi namna walivyoshughu-likia suala hilo kitafanyikaMarch 18,mwaka huu.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment