NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

MSD yaombewa msamaha wa kodi

 
 KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi, imeiomba Serikali kutoa kibali cha msamaha wa kodi bandarani kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuondoa changamoto ya uingizaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi.

Kauli hiyo ya Kamati, imekuja baada ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu kuieleza kamati hiyo changamoto wanazokutana nazo katika uingizaji wa dawa kutoka nje ya nchi na kwamba dawa hizo zinapofika bandarini huchelewa kuzipata kutokana na mfumo wa ulipaji kodi.

Alifafanua kwamba MSD huagiza dawa na vifaa tiba kwa asilimia 80, kutoka nje na hiyo ni kwa sababu ya uwezo mdogo wa viwanda vya ndani kwa kuzalisha dawa zisizo na ubora hivyo zinavyofika hushindwa kuzipata kwa wakati kutokana na kodi. Kutokana na hali hiyo, alisema hushindwa kufika kwa wakati na kusababisha ukosefu wa dawa pindi zinapohitajika.

Baada ya maelezo hayo, wajumbe wa kamati hiyo walihoji kama serikali inatoa vibali kwa misamaha ya kodi kwa taasisi za dini, ni vyema pia kuangalia jinsi ya kutoa kibali hicho kwa MSD ili kusaidia dawa kuingia kwa wakati nchini na kuhudumia Watanzania.

Mjumbe wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alisema serikali inatakiwa kulifuatilia jambo hili kwa kuwa wanaoathirika ni wananchi ambao ndio walipa kodi.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hasna Mwilima alisema kupitia kamati hiyo, watapeleka hoja hiyo bungeni kuhakikisha jambo hilo linafanyika ili kunusuru usumbufu ambao MSD wanaupata.

chanzo>msama
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment