Serikali
ya Tanzania imetoa tamko kuwa kwa sasa haina mpango wowote wa
kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa ambayo yametokana na vitendo
vya ujangili na vifo asilia vya tembo.
Tamko
hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof.
Jumanne Maghembe akizungumza na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark
Childress alipotembelewa na balozi huyo ofisini kwake kujadili maendeleo
ya sekta ya Maliasili mchini.
Prof.
Maghembe alisema hayo baada Balozi huyo wa Marekani hapa nchini kutoa
pendekezo kwa Serikali ya Tanzania kuchoma sehemu meno ya tembo
yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu ya dhamira ya
Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.
"Naomba
niweke wazi kuwa kwa sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya, tunaweza
kuyatumia kwenye tafiti za kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za
ujangili ambazo zipo mahakamani na nyingine ambazo bado zinafanyiwa
uchunguzi" Alisema Prof. Maghembe.
Zipo
nchi mbalimbali duniani ambazo zimechukua hatua ya kuteketeza meno yake
ya tembo yaliyohifadhiwa ikiwemo nchi jirani ya Kenya na Malawi ambapo
inaaminika kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kushawishi Ulimwengu
kukomesha biashara hii haramu ya meno ya tembo.
Nchi
nyingine ni Chad, Ubelgiji, Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno.
Kwa upande wa nchi ambazo zina msimamo sawa na Tanzania katika kuendelea
kuhifadhi meno yake ya Tembo ni pamoja na Afrika ya Kusini, Botswana na
Zimbabwe.
Akizungumzia
kuhusu kuendeleza sekta ya Maliasili nchini, Prof.Maghembe amemuomba
Balozi wa Marekani Bw. Mark Childress kushirikiana na Serikali ya
Tanzania katika kukuza sekta hiyo kwa kuleta wawekezaji mbalimbali
kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia kwenye
mapambano dhidi ya Ujangili.
Aliongeza
kuwa Tanzania ina fursa nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa
ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za kisasa na kuendeleza vivutio
mbalimbali vilivyomo hapa nchini.
Prof.
Maghembe amemshukuru balozi huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali
ya Marekani ya kuendeleza sekta ya Maliasili nchini ukiwemo wa hivi
karibuni wa mbwa maalum (Snifer Dogs) kwa ajili ya kusaidia utambuzi wa
rasilimali za Maliasili zinazoweza kutoroshwa nje ya nchi kupitia
bandari na viwanja vya ndege.
Katika
taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao baina ya Waziri wa Maliasili Prof.
Jumanne Maghembe na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress
imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali ya
Marekani imetoa misaada mbalimbali ambayo jumla yake ni dola za
kimarekani Milioni 41.35 katika kusaidia eneo la uhifadhi hapa nchini.
Akizungumzia
mahusiano baina ya Tanzania na Marekani Balozi Mark Childress
alimueleza Prof. maghembe kuwa Serikali ya Marekani itaendeleza
mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ambapo pia ofisi yake
ya ubalozi imeshatafuta wadau mbalimbali ambao wapo tayari kusaidia
fedha, vifaa na mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na mapambano
dhidi ya ujangili.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment