Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe amepokea taarifa ya
utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kutoka Tume ya
kurekebisha Sheria.
Akipokea
taarifa hiyo leo Jijini Dar es salaam Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe
amesema taarifa hiyo ya utafiti itasaidia kurekebisha sheria ya manunuzi
ambayo inalenga kukuza uchumi wa nchi.
“Mimi
na wataalamu wangu tumeipokea taarifa hii, tutaiangalia na kuhakikisha
tunaifikisha Wizara ya Fedha na Mipango na kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ili kuendelea na utaratibu unaofuata ili mchakato wa
marekebisho uweze kufanyika kwa haraka”alisema Dkt Mwakyembe.
Mwenyekiti
wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius Mujulizi (Kushoto)
akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya utafiti wa marekebisho ya
Sheria ya Manunuzi ya Umma, katikati ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Dkt.Harrison Mwakyembe na kulia ni katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof.
Sifuni Mchome.
Akifafanua
juu ya sheria ya manunuzi ya Umma, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha
Sheria Jaji Aloysius Mujulizi amesema kuwa Tume imefanya utafiti wa
sheria hiyo kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
“Tumepata
maoni mengi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wasimamizi wa
manunuzi ya Serikali kwa namna wanavyoiona sheria ya manunuzi ya Umma,na
sisi tumeyachambua maoni hayo kwa kutumia vigezo vya sheria”alisema
Jaji Mujulizi.
Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza mara baada
ya kupokea taarifa ya utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya
Umma kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius
Mujulizi na kulia ni katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Sifuni Mchome.
Aidha,Tume
imetoa maoni kwa Serikali kusimamia sheria ili iweze kuendana na ukuaji
wa uchumi nchini kwa kurekebisha baadhi ya sheria ili kuepuka
muingiliano uliopo kati ya sheria ya manunuzi na sheria nyingine.
Marekebisho
ya sheria hii ni moja ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli lililotolewa Novemba 2015
alipokua akizindua Bunge la 11.
Imeandaliwa na Jacquiline Mrisho -MAELEZO
0 comments:
Post a Comment