Jeshi la Polisi limeendelea na
kamatakamata ya wapinzani wa vyama vinavyounda Ukawa katika maeneo mbalimbali
likieleza sababu tofauti za kijinai zinazohusishwa na masuala ya kisiasa.
Mpaka sasa wabunge wa upinzani
waliokamatwa ni; Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga) na Peter
Lijualikali (Kilombero), wote wa Chadema na baadhi ya madiwani wa chama hicho
katika Jiji la Dar es Salaam.
Vilevile, imeelezwa kuwa Mbunge
wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alikuwa anatafutwa kuunguanishwa na wenzake.
Pia, baadhi ya wanasiasa wa CUF
Zanzibar wamekamatwa na kuhojiwa kwa madai ya kuwatusi viongozi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Viongozi wa CUF waliohojiwa na
polisi mpaka sasa ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Ali Shehe na
Kiongozi wa Mkakati wa Ushindi, Mohamed Sultan Mugheir ‘Eddy Riyami’ ambaye
yuko nje kwa dhamana.
Mbali na viongozi hao, Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui jana amepatiwa barua ya wito
na Polisi Zanzibar ikielezwa kuna mambo yanamhusu.
Hii ni mara ya pili kwa Mazrui
kuitwa polisi tangu kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, huku CUF ikidai kuwa huo
ni mwendelezo wa mkakati maalumu dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari
na Uhusiano wa Umma wa CUF, Maalim Hamad Masoud Hamad alidai kuwa hatua hiyo ni
utekelezaji wa maagizo ya kisiasa ya kutaka kumkamata kila kiongozi wa juu wa
CUF kuelekea uchaguzi wa marudio.
“Kwa viongozi wa CUF hili
halishangazi, nahisi ingelikuwa ni hatua ya kushangaza sana iwapo wanaoitwa kuhojiwa na polisi ni
viongozi wa vyama vingine.
"Sisi upande wetu hili ni
jambo la kawaida mno na watu wasishangae,” alisema.
Mazrui ambaye pia alikuwa Waziri
wa Biashara na Uwekezaji, ametakiwa kuripoti Makao Makuu ya Polisi, Ofisi ya
Upelelezi Ziwani mjini hapa kesho saa 2.00 asubuhi na kuonana na mkurugenzi wa
makosa ya jinai Zanzibar.
Polisi Zanzibar imethibitisha
kuwapo wito huo ikisema kuna mambo muhimu yanayomhusu mwanasiasa huyo
CHANZO:MPEKUZI
0 comments:
Post a Comment