Newspointtz.blog
RAIS
wa Vietnam, Truong Tan Sang anatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ziara
rasmi ya kiserikali akifuatana na mke wake Mai Thi, mawaziri watano na
wafanyabiashara 51.
Hii
ni ziara ya kwanza ya Mkuu wa nchi kuzuru nchini tangu Rais John
Magufuli aingie Ikulu, lakini pia itakuwa ziara ya kwanza kwa Rais
Truong kuzuru Afrika na Tanzania na baadaye ataelekea Msumbiji.
Pamoja
na kuwa na mazungumzo na Rais Magufuli, Rais Truong atakutana na
Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Rais wa
Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Spika wa Bunge Job Ndugai na kushiriki
dhifa ya kitaifa Ikulu.
Atakapowasili
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam saa 2.30 usiku
kesho, Rais Truong atapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga.
Mapokezi
rasmi kwa Rais huyo yatafanyika Jumatano Ikulu, Dar es Salaam ambapo
kama zilivyo taratibu za kidiplomasia duniani, atapigiwa mizinga 21 na
kukagua gwaride rasmi la Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Mahiga alisema baada ya
kupokelewa Ikulu na Rais Magufuli, kupigiwa mizinga na kukagua gwaride,
Rais Truong atakuwa na mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais
Magufuli.
“Baada
ya mazungumzo waheshimiwa marais watahudhuria hafla ya utiaji saini
Mkataba wa masuala ya Kodi. Mkataba huu lengo lake ni kuchochea biashara
baina ya Vietnam na Tanzania ambapo wafanyabiashara wa nchi zetu mbili
hawatatozwa kodi mara mbili kwa biashara na uwekezaji watakaoufanya,” alisema Balozi Dk Mahiga.
Alisema
saa tano kesho, Rais Truong na ujumbe wake watakwenda katika Ofisi
Ndogo ya CCM Lumumba kwa ajili ya kukutana na Kikwete na kufanya
mazungumzo, hasa kutokana na Rais Truong kuwa pia ni mmoja wa viongozi
waandamizi wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam ambacho kina uhusiano wa
muda mrefu na CCM.
Kwa
kuzingatia mabadiliko makubwa katika uhusiano wa kimataifa ambapo dunia
sasa inatupia macho zaidi kwenye diplomasia ya uchumi, baada ya kutoka
Lumumba, Rais huyo atakwenda katika eneo maalumu la uwekezaji la EPZA
Ubungo ambapo atapata fursa ya kutembelea viwanda na kupata taarifa za
fursa za uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini.
“Saa 9:00 kamili jioni, Rais Truong na ujumbe wake watahudhuria Mkutano wa Biashara na Uwekezaji baina ya Vietnam na Tanzania.
"Saa
11 jioni atakutana na Spika wa Bunge Ndugai, saa 12.30 atakutana na
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Shein na saa 1
jioni atahudhuria Dhifa ya Taifa, itakayoandaliwa kwa heshima yake na
Rais Magufuli,” alisema Dk Mahiga.
Kwa
mujibu wa Dk Mahiga, Alhamisi Machi 10, Rais Truong na ujumbe wake
watakuwa na ratiba ya kutembelea mbuga za wanyama kati ya Saadani na
Serengeti na Ijumaa Machi 11, Rais Truong na ujumbe wake wataondoka
nchini kuelekea Msumbiji.
Katika ujumbe wake, Rais huyo atafuatana na mawaziri watano; wa Viwanda, Kilimo, Mawasiliano, Afya na Maji.
Uhusiano wa Tanzania na Vietnam
Balozi
Mahiga alisema uhusiano wa Tanzania na Vietnam ulianza miaka ya 1960
wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati
Vietnam ikiwa chini ya chama tawala cha Kikomunisti na Tanzania chini ya
TANU (baadaye CCM) na kufanya kwa kiasi kikubwa nchi hizo kuwa na mambo
yanayofanana kichama na kiserikali.
Alisema
ikiwa nchi masikini kama Tanzania, Vietnam ilianzisha mapinduzi makubwa
ya kuuhuisha uchumi wake ili kufikia uchumi wa kati, na katika miaka
15, uchumi wa nchi hiyo ulizaa miujiza, baada ya pato la mwananchi
kutoka Dola 100 kwa mwaka hadi kufikia Dola 2,000 na kuwa mfano wa
kuigwa kwa mataifa yanayoendelea Asia na Afrika.
Ikiwa
na ukubwa wa mita za mraba 330,000 ambao ni sawa na theluthi ya ukubwa
wa Tanzania, ina idadi kubwa ya watu wanaofikia milioni 91 lakini
Vietnam imefanikiwa kuwa nchi ya juu kabisa kwa uuzaji wa kahawa aina ya
Robusta na korosho duniani na inaongoza kwa ufugaji wa samaki.
“Kinacholeta
upekee hapa ni kwamba mbegu ya kahawa ya wa-Vietnam waliichukua hapa
Tanzania mkoani Kagera, halafu mbegu ya korosho waliichukua Mtwara na
mbegu ya samaki wanaotamba nao aina ya tilapia walichukua katika Ziwa
Victoria,” anasema Waziri Mahiga.
Waziri
Mahiga akizungumzia maendeleo katika mawasiliano anaitaja kampuni ya
Viatel ambayo imepiga hatua kubwa ya mawasiliano duniani, Tanzania
ikiendesha huduma zake kupitia mtandao wa mawasiliano wa Hallotel ambao
ni maarufu zaidi katika maeneo ya vijijini kutokana na kutoa huduma za
intaneti bure.
Vita ya Vietnam na Marekani
Pengine
jambo la haraka sana la kuwawezesha Watanzania kuifahamu Vietnam ni
kuzungumzia vita ya Vietnam na Marekani, hasa kutokana na mabanda mengi
yanayoonesha mikanda inayohusiana na vita jijini Dar es Salaam na katika
miji mingi nchini kupenda zaidi kuonesha vita ya Vietnam na Marekani.
Chimbuko
la vita ya Vietnam na Marekani, lilitokana na hatua ya nchi hiyo
kugawanyika Kaskazini na Kusini mara baada ya Uhuru wake mwaka 1945,
ambapo waasi wa Kusini walitaka kujitenga, hatua iliyosababisha serikali
ya Kikomunisti kuamua kupigana ili kurejesha taifa moja.
Kutokana
na kuzuka kwa vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe, Marekani iliamua
kuingilia kati ili kuwasaidia waasi wa Vietnam Kusini wakijulikana zaidi
kama Saigon, kabla ya kukumbana na kichapo kikali kutoka kwa Serikali
ya Kikomunisti chini ya Jenerali maarufu Giap Nguyen huku askari wake
56,000 wakiuawa.
Waziri
Mahiga alisema nidhamu, juhudi, maarifa na kutokubali kushindwa kama
inavyoonesha katika mkanda huo wa vita, ndio chimbuko la mafanikio
makubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo.
“Tunajifunza
mambo matatu makubwa kutoka Vietnam; Moja uwezo mkubwa wa kufanya kazi
kwa bidii hata iwe katika mazingira magumu ikiwemo vita au amani.
“Pili;
ni watu wa utekelezaji na tatu ni uwezo wa kujibu swali; kwamba kama
unataka kuendelea unahitaji nini, kwanza ni elimu ya ufundi, halafu
miundombinu kama vile barabara, umeme, reli, maghala na mwisho mitaji ya
kifedha, na hasa mapinduzi makubwa katika sekta ya benki ili kupata
mikopo,” alisema Waziri Mahiga.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment