Wakuu wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameikubalia Sudan Kusini kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.
Mkutano wa kilele wa Jumuiya hiyo jijini Arusha leo
Jumatano (Machi 2) umepitisha pendekezo la baraza la mawaziri juu ya
uwanachama wa Sudan Kusini na pia hali ya usalama nchini Burundi.
Kikao hicho kilichodumu kwa muda wa takribani masaa matano kimelikubalia
taifa hilo changa kabisa barani Afrika kuwa mwanachama wake wa sita,
kuungana na Tanzania, Rwanda, Burundi , Uganda na Kenya.
Rais Magufuli ambaye ndiye mwenyekiti wa kikao hicho, amewaambia wajumbe wa mkutano huo wa kilele kwamba sasa "Sudan ya Kusini ni mwanachama halali wa jumuiya" hiyo.
Mkutano huo pia umezungumzia
kwa kina masuala ya maendeleo ndani ya jumuiya ikiwemo mipango ya
kujengwa kwa viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi ili kuondoa kabisa
biashara ya uagizaji wa nguo kuukuu, maarufu kama mitumba, katika nchi
hizo katika miaka michachache ijayo
Mkutano huo pia umeshuhudia
uzinduzi wa pasi ya kusafiria ya kielektroniki itakayotumiwa katika
eneo la Afrika Mashariki pamoja na mwongozo maalum wa kimaaadili katika
biashara kwenye nchi wanachama wa jumiya hiyo.
Akizungumzia
kuhusu maendeleo ya jumuiya hiyo, Katibu Mkuu anayemaliza muda wake,
Dk. Richard Sezibera, amesema kuwa jumiya hiyo inasonga mbele kwani
itifaki mbalimbali zimepitishwa kuanzia ushirikiano katika soko la
pamoja, ushuru wa forodha na sasa wanaelekea kufikia hatua ya Afrika
Mashariki kuwa na sarafu moja itakayotumika katika nchi zote wanachama.
Amesema
kuwa tayari jitihada zinaendelea katika kuondoa vikwazo mbalimbali
katika sekta za mawasiliano, biashara na usafiri "ili kuwapa wananchi wa
Afrika Mashariki fursa ya kuufurahia na kufaidi muungano" huo.
Katika
mkutano huo, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi hakuhudhuria na badala
yake alimtuma makamu wake wa pili, Joseph Butore, huku serikali ya Sudan
Kusini ikiwakilishwa pia na makamu wa pili wa rais, James Waniiga.
Na katika hatua nyingine kikao hicho kimepitisha jina la Liberate Mfumukeko kutoka Burundi kuwa katibu mkuu mpya wa jumuiya hiyo kuanzia Aprili 1 mwaka huu.
SourceMpekuzi
0 comments:
Post a Comment