Waziri
wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni amesema ameridhishwa na
eneo lililotengwa kwa ajili ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa bomba la
kusafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert hadi Bandari ya Tanga.
Alitoa
kauli hiyo jana alipoongoza ujumbe wa wataalamu na wawekezaji kutoka
mashirika ya TOTAL, TULLOY na CNOOC ambayo yanatarajiwa kutekeleza
ujenzi wa mradi huo; na kutembelea maeneo utakapojengwa mradi wa bomba
la mafuta ghafi katika Bandari ya Tanga.
Muloni
alisema baada ya kupata maelezo ya kina na kutembelea Bandari ya Tanga
ameridhishwa na mazingira yaliyopo na kwamba wiki ijayo Serikali ya
Uganda itatuma timu ya wataalamu watakaokagua maeneo yote yatakapopita
mabomba na ujenzi wa matangi ya kuhifadhia ili kujionea hali halisi
kabla ya kuruhusu mradi kuanza kutekelezwa.
“Nimeona
taarifa ya mradi iliyowasilishwa hapa na wataalamu na pia nimepata
fursa ya kutembelea Bandari ya Tanga na kimsingi nimeridhika na wiki
ijayo nitatuma timu ya wataalamu ili kuja kufanya uhakiki na kushauri
kabla ya utekelezaji rasmi kuanza,” alisema Muloni.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Justin Ntalikwa alisema
amefurahishwa na ujio wa ujumbe huo ambao utarahisisha uamuzi wa
kujengwa mradi huo nchini hasa baada Serikali ya Kenya kuanza kushawishi
mradi huo ufanyike nchini humo.
“Tumethibitisha
kwamba kupitia bandari hii ya Tanga tunavyo vigezo vya kuweza
kutekeleza mradi huu hasa ikizingatiwa kwamba tunao mtandao mzuri wa
miundombinu ya reli, barabara na bandari ambayo hata mradi utakapoanza
tutaweza kuleta vifaa kwa urahisi tofauti na wenzetu wa nchini Kenya,” alisema Ntalikwa.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),
Dk James Matarajio alisema mazingira ya Bandari ya Tanga ambayo
inazungukwa na visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na vingine ni salama
zaidi kwa meli kufanya shughuli zake bila kukumbwa na hatari ya mawimbi
makubwa ya bahari.
“Bandari
ya Tanga ni tofauti kabisa na bandari nyingine ambazo zimekwisha
tembelewa kama bandari ya Lamu ya nchini Kenya ambayo haifanyi kazi.
Kwanza ina kina kirefu sana cha zaidi ya mita 40 wakati meli kubwa kama
hizo za mafuta zinahitaji kina cha mita 18 na vile vile Bandari ya Tanga
imeunganishwa na mtandao wa barabara na reli ambao unaweza kusafirisha
mizigo hapa ukaipeleka Dodoma, Mwanza, Burundi hadi Uganda.
“Hivyo
tunatumaini kwamba Serikali ya Uganda itakapokuwa inafanya maamuzi yake
itachukua ruti ya Tanzania kama ambavyo viongozi wetu wa nchi walisaini
makubaliano ya kuutekeleza huu mradi,” alisema Dk Mataragio.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema mkoa huo
umejipanga kupokea mradi huo na ambao utaongeza fursa za kiuchumi kwa
wananchi wa Tanga na Taifa.
Mradi
wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi unatarajiwa kujengwa katika eneo
lililopo kati ya visiwa vidogo vya Fungunyama, Ulenge na Chongoleani
jijini Tanga na unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni nne hadi
kukamilika.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment